Wednesday, July 9, 2014

TCDC YAWATAKA WAHUDUMU WA AFYA KUHAMASISHA JAMII KUZINGATIA MASUALA YA AFYA

Aliyesimama ni mtendaji wa kata ya Kihagara wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, Emmanuely Nkaleka akisisitiza jambo katika mafunzo ya siku mbili ya Wahudumu wa afya watendaji wa vijiji, yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo Mbinga mjini.

Baadhi ya Washiriki wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa na wakufunzi wa mafunzo hayo. (Picha zote na Kassian Nyandindi)

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

IMESISITIZWA kuwa mama mjamzito anatakiwa kwenda kliniki mapema mara baada ya kujitambua kuwa ni mjamzito, ili aweze kujifungua salama na kuepukana na madhara yanayoweza kutokea baadae.

Aidha katika kuleta ufanisi Wahudumu wa afya wilaya ya Mbinga na Nyasa mkoani Ruvuma, wametakiwa kuhamasisha jamii kuona umuhimu wa utekelezaji wa jambo hilo kwa lengo la kuachana na vitendo vya akina mama wajawazito kujifungulia majumbani, badala yake waende kwenye vituo vya afya, zahanati au hospitali.

Rai hiyo ilitolewa leo na Mratibu wa mfuko wa afya ya jamii (CHF) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Alphonce Njawa alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wahudumu wa afya watendaji wa vijiji wa wilaya hizo, ambayo yamendaliwa na shirika lisilo la kiserikali ‘Tanzania Communication and Development Center’ (TCDC) yaliyofanyika katika ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.

Njawa alisema kuwa mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuwapa taarifa za mabadiliko ya kiutendaji na ongezeko la maeneo ya kufanyia kazi, pamoja na kutoa elimu ya afya kwenye jamii kuepukana na tabia hiyo na hatimaye hata kupunguza vifo visivyo vya lazima.


“Ndugu zangu mafunzo haya yanalenga pia huko tuendako tujitahidi kuhamasisha wananchi vijijini kuachana na mitandao ya ngono ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikieneza kwa kasi maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa ukimwi”, alisema.

Alisema Wahudumu hao hawana budi kuzingatia maagizo watakayopewa, ambayo yataleta mabadiliko chanya katika jamii na hatimaye kuweza kufikia malengo ya kupunguza tatizo la maambukizi ya ugonjwa huo.

Kwa upande wake Meneja wa mkoa wa Ruvuma wa TCDC Assely Mwamaka alisema shirika hilo limekuwa likijikita katika shughuli zake kwenye maeneo matatu ambayo ni kutokomeza ugonjwa wa malaria, kuongeza matumizi ya uzazi wa mpango na kuzuia maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi.

Mwamaka alieleza kuwa maeneo hayo yanalenga kutatua matatizo ya msingi kuhusu afya ya jamii, ambayo yameendelea kuwa mzigo mkubwa kwa familia au kaya hapa nchini.

Vilevile aliwataka Wahudumu hao wa afya huko vijijini waende kuelimisha wazazi wenye vyandarua vya ziada wawapatie wenzao ambao hawana vyandarua, na sio kubaki navyo majumbani mpaka kufikia hatua ya kuharibika au kufanyia matumizi ambayo sio sahihi.

Alisema baadhi ya maeneo hapa mkoani Ruvuma, kumekuwa na tabia ya watu kutumia vyandarua kwa matumizi ambayo sio sahihi kama vile kuzungushia uzio wa bustani au kufanyia shughuli za uvuvi wa dagaa, katika maeneo ya mwambao mwa ziwa Nyasa jambo ambalo ni kinyume na taratibu zilizowekwa.

Kufuatia hali hiyo Meneja huyo aliwaagiza watendaji wa kata kuwachukulia hatua watu wanaofanya hivyo, ili kuweza kudhibiti vitendo hivyo ambavyo havileti picha nzuri katika jamii.

No comments: