Tuesday, July 22, 2014

HALMASHAURI NCHINI ZAAGIZWA KUONGEZA VYANZO VYA MAPATO

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

RAIS  Dokta Jakaya Kikwete ameziagiza Halmashauri za wilaya na Manispaa hapa nchini, kuongeza vyanzo vipya vya mapato badala ya kutegemea wafadhili na serikali kuu.

Akihutubia mkutano wa hadhara mara baada ya kufungua soko la kimataifa la Mkenda ambalo ujenzi wake umegharimu shilingi milioni 169 na ambalo lipo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji, wilaya ya Songea mkoani Ruvuma alisema viongozi na watendaji wasipokuwa wabunifu katika kuongeza vyanzo vipya vya mapato hawataweza kusonga mbele kimaendeleo.

Kikwete alisema halmashauri nyingi zimekuwa zikitegemea chanzo kimoja cha mapato, hususan fedha zinazotolewa na serikali kuu jambo ambalo husababisha utekelezaji wa baadhi ya miradi ya wananchi kukwama.

Alisisitiza juu ya umuhimu wa watendaji na madiwani kusimamia fedha zinazotolewa na serikali ipasavyo, kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili iweze kukamilishwa kwa viwango vinavyotakiwa.

Dhamira ya serikali ni kuhakikisha katika maeneo ya mipakani inafanyika biashara halali, ambapo ili kuweza kupata mafanikio masoko hujengwa na kuwafanya wananchi wa pande zote mbili waweze kufanya biashara.

"Tunafanya hivi kwa mikoa yote ya mipakani na kukamilika kwa ujenzi wa soko hili la Mkenda kutawafanya wananchi wa hapa kwetu na wa Msumbiji, kuanza kufanya biashara kwa uhakika kutokana na kuwa na mahali pazuri pa kukutana,"alisema Kikwete.

Dokta Kikwete aliwataka wananchi wa kata ya Mhukuru ambayo ipo mpakani mwa Msumbiji kuendelea kudumisha uhusiano uliopo baina ya nchi hizo mbili, na kwamba pale wanapotaka kuingia upande wa pili wazingatie sheria zilizowekwa ili wasipatwe na matatizo.

Katika hatua nyingine Rais aliwataka maofisa ardhi nchini waelimishe wananchi ili waweze kujitokeza kwa wingi, kupata hati miliki za kimila ili waweze kuwa na uhakika wa kukopesheka na vyombo vya fedha kama vile benki.

Hata hivyo aliwataka wale ambao wanapata hati miliki za kimila kutumia vizuri mikopo wanayokopeshwa, na kwamba lengo la serikali kuhakikisha hati hizo zinatambulika kisheria kimsingi ililenga watu wa chini ambao wanakuwa hawana sifa za kukopa benki hasa waishio maeneo ya vijijini.

No comments: