Monday, July 7, 2014

KUNDI LA SIMBA LADAIWA KUVAMIA MIFUGO YA WANANCHI NAMTUMBO


Na Steven Augustino,
Namtumbo.

KUNDI kubwa la Simba limeripotiwa kuvamia na kuanza kuua ng’ombe wa wafugaji katika vijiji vilivyopo kata ya Lusewa wilayani Namtumbo mkoani  Ruvuma,  hali ambayo imewafanya wamiliki wa mifugo hiyo kuishi kwa wasi wasi.

Awali wanakijiji hao walikuwa wakidhani kwamba mifungo yao kuwa ni wezi ndio wanaoiba, kutokana na kutojua ni nani anayehusika na upotevu wa mifugo yao.

Hayo yamebainishwa na Mtendaji wakata ya Lusewa Abdallah Maniamba wakati alipokuwa akizungumza waandishi wa habari juu ya matukio hayo na kuongeza kuwa,  hali hiyo inatokana na ofisi yake kupokea taarifa kutoka  kwa mwananchi  mmoja  aliyejitambulisha kwa jina la Habari  Jamwana kuwa hivi sasa kuna kundi kubwa la simba waliovamia katika maeneo yao na wanamaliza mifugo.

Maniamba alifafanua kuwa aliwaona simba watatu dume, jike na mtoto wakinywa  maji katika  mto  chimalilo wakati  akiwa anaoga maji.


Alisema kufuatia hali hiyo alilazimika kuacha  kuoga na kukimbia kwa kasi baada  ya kuwaona  simba hao wakinywa maji katika  eneo  hilo na  kwenda  nyumbani, hatimaye kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali ili wawajulishe wananchi wao juu ya maeneo yao kuvamiwa na wanyama hao.

Akizungumzia hali hiyo afisa  mhifadhi  wa  wanyama  pori tarafa ya Sasawala Hussein Sudi  mbali na kukiri kuwa na taarifa hizo alisema kuwa  upo ushahidi  wa  kutosha  kuwa,  katika eneo hilo kuna makundi ya  simba  ambao kwa sasa wameripotiwa kuwa wanamaliza  mifugo.

No comments: