Tuesday, July 22, 2014

RAIS JAKAYA KIKWETE AWA MBOGO, AMUAGIZA MKUU WA MKOA WA RUVUMA KUWAKAMATA NA KUWAFIKISHA MAHAKAMANI WALIOHUSIKA NA WIZI WA FEDHA ZA WAKULIMA

Na Kassian Nyandindi,

Namtumbo.

RAIS Jakaya Kikwete amemuagiza Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu ahakikishe kwamba anawakamata na kuwafikisha Mahakamani wale wote ambao wamehusika kwa namna moja au nyingine, kufanya ubadhirifu wa fedha za wakulima wa tumbaku wilaya ya Songea na Namtumbo mkoani humo.

Aidha agizo hilo limefuatia baada ya Mwambungu kuunda tume ya kuchunguza tatizo hilo, ambayo inaendelea kufanya kazi ya ukaguzi wa hesabu za fedha kwa chama cha ushirika wa wakulima wanaozalisha zao hilo kutoka kwenye wilaya hizo mbili (SONAMCU).

Kikwete ambaye alionekana kukerwa na kitendo hicho na kufikia hatua ya kutoa agizo hilo, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa, katika mkutano wa hadhara wa wananchi uliofanyika mjini hapa.


Mbunge huyo alimnyoshea kidole Mrajisi wa vyama vya ushirika mkoani Ruvuma Watson Nganiwa kwa kushirikiana na maofisa ushirika wenzake, wanadaiwa kushiriki katika kufanya ubadhirifu wa mamilioni ya fedha huku wakulima wa tumbaku wakiendelea kubaki kuwa masikini.

Alisema licha ya tatizo hilo kuonekana kuwa sugu kutokana na kudumu kwa miaka mingi sasa, imefikia hatua wakulima wa zao hilo wamekatishwa tamaa kuendelea na kazi ya kilimo hicho kutokana na fedha zao kuibwa mara kwa mara na wajanja wachache.

Kawawa alifafanua kuwa ni jambo la kushangaza kwa mtumishi wa umma kuona anawaibia wakulima fedha zao, wakati amepewa dhamana na serikali ya kuhakikisha anasimamia ipasavyo mali za umma.

“Mheshimiwa Rais viongozi wa ushirika ngazi ya mkoa wana matatizo wamekuwa wakiiba fedha za wakulima hata hawaoni aibu, huku mkulima huyu akiendelea kuteseka kila siku kwa jembe la mkono”, alisema.

Katika hatua nyingine Rais Kikwete alisikitishwa pia na matokeo mabaya ya kumaliza elimu ya msingi na sekondari wilayani Namtumbo, ambapo wilaya hiyo katika kipindi cha mwaka 2012 na 2013 imeendelea kufanya vibaya.

Matokeo mabaya ya ufaulu watoto wa shule za msingi na sekondari katika wilaya hiyo, kunatokana na kukithiri kwa tatizo la utoro na watoto wa kike kupewa mimba huku wahusika kutochukuliwa hatua stahiki za kinidhamu ili kuweza kudhibiti hali hiyo.

Taarifa ya maendeleo ya wilaya hiyo inasema kuwa wanafunzi 4509 waliomaliza darasa la saba mwaka 2013 walikatisha masomo yao kutokana na kuwa na ujauzito, huku wanafunzi 3015 wakishindwa kumaliza masomo yao kufuatia kuwepo kwa tatizo la kutohudhuria masomo darasani (utoro).

Vilevile kwa upande wa shule za sekondari kwa mwaka huo, wanafunzi 1742 hawakumaliza kidato cha nne kutokana na tatizo la utoro huku 997 wakiwa na mimba.

No comments: