Monday, July 7, 2014

TUNDURU KUPATA HATI CHAFU KUTOKANA NA KUTOTEKELEZA IPASAVYO MIRADI YA MAENDELEO YA WANANCHI


Na Steven Augustino,
Tunduru.

HALMASHAURI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma huenda ikapata hati chafu katika mwaka huu wa fedha, kutokana na halmashauri hiyo kutotekeleza ipasavyo ujenzi wa miradi 16 ya maendeleo ya wananchi kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014 yenye thamani ya shilingi milioni 284.3.  

Mwakilishi wa mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali mkoani Ruvuma, Leonard Chama alisema kuwa tatizo hilo linatokana na halmashauri hiyo kushindwa kusimamia ipasavyo ujenzi wa zahanati, madarasa, visima vya maji na ofisi ya kata.

Kufuatia hali hiyo Baraza la madiwani la halmashauri hiyo limesikitishwa na hali hiyo na kuutaka uongozi husika wa wilaya ya Tunduru kuhakikisha kwamba makosa hayo hayajirudii tena.


Hayo yalijiri katika kikao cha dharula cha baraza hilo kilichoketi kwenye ukumbi wa Klasta ya walimu tarafa ya Mlingoti mjini hapa, baada ya kutolewa kwa taarifa ya Mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali ambapo ilionesha kuwa miradi ya maendeleo ya wananchi wilayani humo utekelezaji wake, umekuwa ni wa chini ya kiwango na haukidhi mahitaji halisi.

Awali katika ufunguzi wa kikao hicho Mwanyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru Faridu Khamisi, pamoja na mambo mengine aliwataka madiwani hao kuchangia hoja zao bila uoga na kwamba lengo la kikao hicho ni kupitia na kupitisha hoja hizo za mkaguzi.

Akiwasilisha taarifa ya kamati ya fedha, uongozi na mipango, makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, ambaye ni diwani wa kata ya Mchoteka Mkwanda Sudi alisema kuwa taarifa hiyo ya mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali ilipitiwa na kudadavuliwa ipasavyo hatimaye kubaini mapungufu yaliyopo.

Pia diwani wa kata ya Mlingoti Mashariki Ally Mchemela alielezea juu ya mapungufu yaliyojitokeza, ambapo kulikuwepo ukiukwaji wa taratibu husika kwa Kampuni State business Company Limited iliyopewa zabuni ya kukusanya ushuru wa mazao baada ya kubainika kupoteza vitabu viwili vilivyokuwa vikitumika kukusanyia mapato, kwa halmashauri ya Tunduru huku akiachwa huru bila kuchukuliwa hatua za kisheria.

No comments: