Saturday, July 19, 2014

SERIKALI YAWAHAKIKISHIA WAKULIMA SOKO LA MAHINDI, JK ASEMA SHILINGI BILIONI 15 ZIMETENGWA KUNUNULIA ZAO HILO


Na Kassian Nyandindi,
Songea.

RAIS Jakaya Kikwete amesema serikali imetenga shilingi bilioni 15 zikazotumika kununulia mazao ya wakulima, kupitia wakala wa hifadhi ya chakula ya taifa nchini(NFRA) kuanzia Agosti mosi mwaka huu msimu wa mavuno ya zao la mahindi utakapofunguliwa.

Akizungumza mara baada ya kukagua na kuzindua ghala jipya la hifadhi ya taifa ya chakula, lililopo eneo la Ruhuwiko mjini Songea alisema kuwa ili kuweza kuhifadhi mazao mengi kwa wakati mmoja ni lazima pawe na maghala mengi na ya kisasa.

Alisema hivi sasa taifa lina akiba ya kutosha ya chakula ambapo maghala yake yamejaa mazao, ikiwemo ghala la NFRA la mjini hapa ambapo kuna tani 51,000 ambazo bado hazijaondolewa huku wakati wa kununua mazao mapya ukiwa umewadia.


Kikwete alisema kuwa mpango unaendelea kufanyika ili mahindi yaliyopo yaweze kuuzwa katika nchi ambazo zina upungufu mkubwa wa chakula ikiwemo Kenya,Sudan Kusini na shirika la WFP ambapo kwa kufanya hivyo maghala yaliyofura mazao yatakuwa wazi na kuweza kupata nafasi ya kuweka mazao yatakayonunuliwa.

Alisema serikali itaendelea kuiwezesha NFRA ili iweze kununua mazao ya wakulima jambo ambalo litasaidia kuwapatia bei nzur, na hivyo kuepukana na wafanyabiashara walanguzi ambao siku zote wamekuwa na kawaida ya kuwaibia kutokana na kununua mazao yao kwa bei ya chini.

Rais aliwataka wakulima kutokuwa na haraka ya kuuza mazao yao kwa walanguzi hao, badala yake wasubiri msimu ufunguliwe na kwamba alisisitiza juu ya umuhimu wa kujiunga pamoja na kuanzisha vikundi vya ujasiriamali jambo ambalo pia litapelekea wauze mazao yao kwa pamoja.

Awali katika taarifa yake Naibu waziri wa kilimo na chakula Godfrey Zambi alisema NFRA inahitaji kiasi cha shilingi bilioni 211, kwa ajili ya ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao ya chakula na kwamba mpaka sasa kuna maghala 31 nchini kote.

Zambi alisema kuwa lengo la serikali ni kununua tani 400,000 ifikapo mwaka 2016/17 hivyo ili kufanikisha zoezi hilo, jitihada kubwa zinapaswa kufanyika kufanikisha ujenzi wa maghala hayo ambayo yatatumika kuhifadhia mazao baada ya kununua kutoka kwa wakulima.

Wakati huohuo Rais Jakaya Kikwete amesema rushwa imeshamiri katika kitengo cha manunuzi jambo ambalo limekuwa likisababisha miradi mingi ya kimaendeleo ishindwe kukamilika kwa viwango vinavyotakiwa, na kuiagiza taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa(TAKUKURU)ihakikishe inafuatilia kwa umakini eneo hilo.

Akizungumza mara baada ya kufungua ofisi ya TAKUKURU mkoani Ruvuma iliyojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.1 alisema matumizi mabaya ya madaraka na fedha za umma zinazoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo, haiwezi kufumbiwa macho hivyo jitihada za makusudi zinapaswa kufanyika ili kukabiliana na wale wote wenye tabia hiyo inayorudisha nyuma jitihada za serikali za kuwaletea wananchi maendeleo.

Kikwete alisema kuwa serikali inathamini kazi kubwa zinazofanywa na TAKUKURU hivyo itaendelea kuwajengea uwezo ili waweze kupata mafanikio makubwa, katika utendaji wao na kwamba elimu kwa umma ni muhimu kuendelea kutolewa jambo ambalo litaifanya jamii kuweza kutoa ushirikiano kwao.

Aliiasa taasisi hiyo kutokubali kunyooshewa kidole na wananchi kwa kuchelewa kuchukua hatua katika maeneo yale ambayo wanakuwa wamepata taarifa ihisuyo matumizi mabaya ya fedha za serikali, na kwamba katika kuhakikisha kazi yao inakuwa rahisi serikali itahakikisha inaongeza idadi ya watumishi,vitendea kazi na kuendelea kujenga ofisi tatu kila mwaka.

Katika hatua nyingine Rais Kikwete amefungua mradi wa nyumba za gharama nafuu mjini hapa ambazo zimejengwa na shirika la nyumba za taifa(NHC) ambapo zimejengwa nyumba 18 ambazo mpaka kukamilika kwake zitagharimu shilingi milioni 676.2

Aliwaleleza wananchi mara baada ya kufungua nyumba hizo Rais alizitaka halmashauri za wilaya na manispaa kote nchini kuhakikisha zinatenga maeneo ambayo shirika hilo litajenga nyumba hizo za gharama nafuu, na kwamba pindi zinapokamilika wananchi wakope fedha katika taasisi za fedha na kununua nyumba hizo ambazo kimsingi zimelenga kuwasaidia wananchi wenye kipata cha chini.

Alilipongeza shirika la nyumba la taifa kwa kuona umuhimu wa kusaidia juhudi za serikali za kutoa ajira kwa vijana kutokana na kitendo chake cha vijana katika halmashauri za wilaya kote nchini kusaidiwa mashine kwa ajili ya kufyatua matofari na kuyauza.

Kikwete alisema utaratibu huo licha ya kuongeza ajira kwa vijana pia utasaidia kubadili sura ya miji kutokana na ukweli kwamba, hakutakuwa na tatizo la upatikanaji wa matofari ya kujengea nyumba za kisasa.

No comments: