Friday, July 18, 2014

KIUNGI MKOMBOZI KWA WANAWAKE MBINGA KATIKA KUMILIKI ARDHI

Mama mmoja ambaye ni Ostina Msuha mkazi wa kijiji cha Ndembo kata ya Linda akiwa katika eneo la ardhi yake yenye zaidi ya ekari mbili kijijini hapo, ambapo iliporwa na hatimaye akafanya jitihada ya kupigania kwa kufuata sheria husika na kufanikiwa kuirejesha mikononi mwake baada ya kupewa elimu na umoja wa kikundi cha maendeleo ya wanawake (KIUNGI) juu ya haki ya mwanamke kumiliki ardhi.

Adelehema Nombo mkazi wa kijiji cha Lituru kata ya Litembo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma akitoa ushuhuda wa eneo la ardhi yake mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) ambayo imeporwa na wajanja wachache kwa muda wa miaka minne na kuuziwa mtu mmoja aliyemtaja kwa jina la Samwel Jaboma mkazi wa Litembo, hivyo baada ya kupewa elimu juu ya haki ya mwanamke kumiliki ardhi ameanza jitihada ya kupigania haki yake kwa lengo la kuirejesha mikononi mwake. (Picha zote na Kassian Nyandindi)
Na Kassian Nyandindi,


Mbinga.

IMEELEZWA kuwa asilimia 95 ya ardhi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, inamilikiwa na wanaume wakati asilimia tano tu ndio humiliki wanawake wachache huku mila na desturi zikiwakandamiza wanawake na kuwanyima fursa, ya kumiliki rasilimali hiyo muhimu.

Sambamba na hilo wanawake sita kati ya 10 wilayani humo ndio ambao huporwa ardhi za mashamba yao na ndugu wa marehemu baada ya kufiwa na mume, hivyo katika kuondokana na tatizo hilo jitihada za makusudi zinapaswa kuchukuliwa ili kuweza kuondokana na hali hiyo.

Kufuatia hali hiyo, umoja wa kikundi cha maendeleo ya wanawake (KIUNGI) wilayani Mbinga umeweza kutambua matatizo hayo yanayowakabili wanawake wilayani humo, katika dhana nzima ya umiliki wa rasilimali ardhi na kuanza kutoa elimu juu ya haki za kundi hilo kumiliki ardhi.


Katika kuharakisha mafanikio ya utekelezaji wa suala hilo, Cecilia Mbata ambaye ni Ofisa ustawi maendeleo ya jamii kitengo cha wanawake wilayani humo, alisema mafunzo ya siku tatu yametolewa ambayo yamefadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali 'The foundation for civil Society', yalishirikisha pia wanaume ili wasiwe pingamizi badala yake wahamasishe jamii ya wanambinga juu ya haki ya mwanamke katika kumiliki rasilimali hiyo.

Alisema kuwa KIUNGI imeweza kutoa mafunzo hayo kwa kuanzia kata mbili za Litembo na Linda wilaya ya Mbinga, ambapo wanawake na wanaume wameweza kuelimishwa na kutambua haki zao za kumiliki ardhi, na sio kuendesha malumbano katika jamii yasiyokuwa ya lazima.

Mbata alisema lengo la kufanya hivyo ni baada ya wanaumoja wa kikundi hicho kutambua na kuona kwamba, wakati umefika sasa kwa mwanamke kujua au kufahamu miongozo, sera na sheria mbalimbali zinazowagusa wanawake katika kutetea mambo yao ya msingi.

Hivyo basi KIUNGI imetambua kuwa pamoja na serikali kuweka mikakati hiyo, lakini walengwa bado hawajui na ndio maana hata utekelezaji wake umekuwa mgumu hususan katika maeneo ya vijijini.

Pamoja na mambo mengine naye Meneja mkuu wa umoja huo Renatha Kapinga, alifafanua kuwa elimu hiyo itaendelea kutolewa kwa wanawake wote wa Mbinga ikiwa ni lengo la kuwafanya waweze kuondokana na mila na desturi kandamizi katika kupata haki zao za msingi juu ya masuala ya kumiliki ardhi.


No comments: