Monday, July 21, 2014

KITUO CHA KISASA MABASI YA ABIRIA MBINGA CHAFUNGULIWA, RAIS APONGEZA UONGOZI WA WILAYA




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta Jakaya Kikwete, akifungua kituo cha kisasa cha mabasi ya abiria Mbinga mjini mkoani Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga. 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta Jakaya Kikwete hatimaye amefanya ufunguzi wa kituo cha kisasa cha mabasi ya abiria ambacho kimejengwa Mbinga mjini mkoa wa Ruvuma, kwa thamani ya shilingi bilioni 2.1.

Fedha za ujenzi wa mradi huo zimetokana na mkopo kutoka bodi ya mikopo ya serikali za mitaa, ambapo majengo pacha ya ghorofa moja yamejengwa yakiwa na vyumba 112 vya kufanyia biashara.

Aidha majengo hayo yana sehemu ya kupumzika abiria, kuegesha magari, miundombinu ya usafi, maji na ya tahadhari ya moto ambapo ujenzi wake umechukua muda wa miezi 39.


Awali akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya Rais Kikwete, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Hussein Ngaga alisema mradi huo umejengwa na kampuni ya GNMS ya kutoka Iringa chini ya usimamizi wa wakala wa majengo hapa nchini (TBA).

“Mheshimiwa Rais lengo la ujenzi wa kituo hiki cha mabasi ni kutoa mazingira mazuri kwa wasafiri wanaoingia na kutoka, kutoa ajira kwa wananchi kwa kuwawezesha kufanya biashara sehemu yenye staha, kuongeza mapato ya ndani ya halmashauri yetu na kuboresha mnadhari ya mji wa Mbinga”, alisema Ngaga.

Ngaga alieleza kuwa halmashauri kwa shughuli zote zitakazo endeshwa katika eneo hilo inatarajia kupata mapato ya shilingi milioni 324.6 kwa mwaka.

Pamoja na mambo mengine Dokta Kikwete aliupongeza uongozi wa wilaya hiyo kuwa wabunifu katika ujenzi wa kituo cha kisasa cha magari ya abria, huku akiwataka wananchi kutunza vizuri mazingira ya kituo hicho ili yawe endelevu na sio kuwa chakavu.

No comments: