Wednesday, July 16, 2014

RAIS JAKAYA KIKWETE KUFANYA ZIARA YA KIKAZI MKOANI RUVUMA, WANANCHI WATAKIWA KUJITOKEZA KWA WINGI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta Jakaya Kikwete.

















Na Kassian Nyandindi,

Ruvuma.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Dokta Jakaya Mrisho Kikwete atafanya ziara ya kikazi mkoani Ruvuma ikiwemo kukagua, kufanya uzinduzi na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya Wananchi mkoani humo. 

Ziara hiyo ni ya muda wa siku saba anatarajia kuwasili katika uwanja wa ndege mjini Songea Julai 17 mwaka huu, majira ya saa tano asubuhi na kupokelewa na uongozi wa mkoa huo.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu ametoa taarifa hiyo leo kwa vyombo mbalimbali vya habari, alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari mjini hapa kwenye ukumbi wa Maliasili wa mkoa huo.

Mwambungu amewataka wananchi waliopo katika maeneo mbalimbali mkoani humo, ambako Rais Kikwete atapita kufanya shughuli hizo muhimu ikiwemo mikutano ya hadhara katika kila wilaya zilizopo hapa mkoani Ruvuma, kujitokeza kwa wingi.


Alisema Rais Kikwete akiwa katika Manispaa ya Songea ataweka jiwe la msingi nyumba bora za gharama nafuu ambazo zimejengwa na shirika la nyumba la Taifa (NHC), Ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ya mkoa wa Ruvuma.

Kadhalika ataendelea na shughuli za ukaguzi na uzinduzi wa ghala jipya la hifadhi ya Taifa ya chakula (NFRA) lililopo mjini Songea, daraja jipya la Ruhekei na mradi wa umeme vijijini (REA) uliopo Mbamba bay wilayani Nyasa.

Pia atafanya ufunguzi wa barabara kuu ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami ya kutoka Mbinga hadi Songea na kituo kikuu cha mabasi ambacho kimejengwa Mbinga mjini.

Rais Kikwete wakati atakapokuwa akiendelea na ziara yake mkoani Ruvuma, atafungua soko la kimataifa la Mkenda ambalo limejengwa mpakani mwa nchi ya Tanzania na Msumbiji ambalo litawanufaisha wananchi wa pande hizo mbili.

Wilayani Namtumbo atafanya uzinduzi wa hospitali ya wilaya hiyo, barabara iliyojengwa kwa kiwango cha lami kutoka Songea hadi Namtumbo.

Uzinduzi rasmi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Namtumbo, Tunduru hadi Sauti moja wilayani Tunduru.

Wilayani Tunduru ataendelea na uzinduzi wa nyumba 40 ambazo zimejengwa na taasisi ya Mkapa foundation zilizopo katika kijiji cha Matemanga na mradi wa maji uliopo tarafa ya Nalasi wilayani humo.

Hata hivyo Rais Kikwete atahitimisha ziara yake Julai 23 mwaka huu, kwa kufanya majumuisho Tunduru mjini na kuondoka wilayani humo kwenda Nachingwea kuelekea Jijini Dar es Salaam.

No comments: