Thursday, September 18, 2014

AHUKUMIWA KWENDA JELA BAADA YA KULAWITI



Na Mwandishi wetu,
Songea.

MKAZI mmoja wa Mjimwema Songea mjini mkoani Ruvuma, amehukumiwa na Mahakama ya Hakimu mkazi wa mkoa huo adhabu ya kifungo cha maisha  kwenda gerezani kwa kosa la kumlawiti msichana mwenye umri wa miaka tisa.

Akisoma hukumu hiyo hakimu mkazi mfawidhi wa mkoa huo, Joakimu Tiganga alisema kuwa mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka kuwa John Mapunda (38) mkazi wa Mjimwema songea mjini bila halali alimlawiti msichana huyo.


Tiganga alisema mahakama imeona kosa alilofanya Mapunda ni la kinyama na hivyo, mahakama imemtia hatiani na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha kwenda gerezani ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Aidha mahakama hiyo imetoa adhabu ya kupigwa viboko 12 na kulipa fedha ya shilingi milioni 2 kwa msichana huyo aliyemtendea unyama huo.

Pamoja na mambo mengine awali  ilidaiwa mahakamani hapo na mwanasheria wa serikali Hamimu Mkoleye kuwa, mshitakiwa Mapunda alitenda kosa hilo la Oktoba 16 mwaka jana akiwa mtaa wa Ruvuma Songea mjini, ambapo alimkamata msichana huyo na kumwingilia kinyume na maumbile.

No comments: