Thursday, September 18, 2014

KATIBU TAWALA MSAIDIZI MKOANI RUVUMA NA WENZAKE WAPANDISHWA KIZIMBANI KWA WIZI WA SHILINGI MILIONI 800

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MWENYEKITI wa chama kikuu cha ushirika (SONAMCU) wilaya Namtumbo mkoani Ruvuma, amefikishwa katika Mahakama ya mkoa huo akiwemo na Katibu tawala msaidizi wa mkoa huo ambaye pia ni afisa ushirika wa mkoa huo, kwa tuhuma za kula njama, kugushi nyaraka na kuiba fedha shilingi milioni 889.

Imedaiwa mahakamani hapo na mwanasheria wa serikali Hamimu Mkoleye mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya mkoa huo Joackimu Tiganga washtakiwa hao wote wawili wanalinganishwa na washitakiwa wengine 14 ambao walikwisha somewa mashitaka na kufanya idadi yao kuwa 16 ambapo wanadaiwa kuiba fedha hizo.

Mkoleye amewataja waliofikishwa mahakamani hapo kuwa ni Ally Athumani Bango (45) Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika Namtumbo (SONAMCO) ambacho kinajishughulisha na ununuzi wa zao la tumbaku.


Mwingine ni Watson Nganiwa (57) Katibu tawala msaidizi ofisi ya mkuu wa mkoa wa Ruvuma, ambaye pia ni Afisa ushirika wa mkoa huo.

Amesema kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa mawili ya kula njama na kugushi nyaraka kisha kufanikiwa kuiba shilingi milioni 889 mali ya vyama vya ushirika.

Kosa hili walilifanya kati ya mwaka 2011-2012 hadi 2013 na kwenda benki kuiba fedha hizo za wakulima.

Washitakiwa wote kwa pamoja wamekana mashitaka na mmoja yuko nje kwa dhamana ambapo Ally Athumani ambaye ni Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika SONAMCO anaendelea kusota mahabusu baada ya kukosa wadhamini wawili wenye sifa hivyo shauri hilo litatajwa tena Oktoba 9 mwaka huu.


No comments: