Thursday, September 18, 2014

ASKARI SONGEA WAJERUHIWA NA KITU KINACHODAIWA KUWA NI BOMU LA KURUSHWA NA MKONO



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

ASKARI watatu  wa Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma, wamelazwa katika hospitali ya mkoa huo iliyopo Songea mjini  wakiwa wanapatiwa matibabu baada ya kushambuliwa na kitu kinachodaiwa kuwa ni bomu la kurusha kwa mkono.

Tukio hilo limetokea Septemba 16 mwaka huu majira ya jioni katika kata ya Msufini mjini hapa, ambapo wamejeruhiwa.

Akizungumzia tukio hilo kaimu kamanda wa polisi wa mkoa huo ASP George Chiposi,  alisema kuwa watu watatu wasio fahamika ndio waliotupa kitu hicho kinacho sadikiwa kuwa ni bomu la kutupwa kwa mkono.

Bomu hilo alisema limetengenezwa kienyeji na kuwajeruhi askari  hao watatu waliokuwa doria.


Kamanda Chiposi aliwataja askari hao waliojeruhiwa kuwa ni  WP. 10399 PC Felista ambaye amejeruhiwa mguu wa kulia  kwenye unyayo na pajani, G. 7351 PC Ramadhani aliye jeruhiwa mguu wa kulia karibu na goti na tumboni upande wa kulia na  G. 5515 pc John aliyepata majeraha katika mguu wa kulia chini ya goti na jeraha dogo tumboni. 

Alisema baada ya tukio hilo majeruhi wote walikimbizwa katika hospitali hiyo ya mkoa,  na wote wamelazwa huko wakiendelea kupatiwa matibabu.

Alifafanua kuwa katika matibabu ya awali waganga (madaktari) wameweza kutoa vipande vya bati na misumari katika majeraha ya askari hao na mpaka sasa wanaendelea vizuri.

Chanzo cha tukio hilo mpaka sasa bado hakijafahamika na akaongeza kuwa uchunguzi wa awali uliofanywa  katika eneo la tukio walifanikiwa kuokota vipande vya chuma, kopo lenye nyaya, kipande cha ganda la betri ambavyo vinasadikiwa ndivyo vilikuwa sehemu ya bomu hilo. 

Kufutia hali hiyo Jeshi la polisi mkoani Ruvuma, linaendelea na uchunguzi  wa ili kuweza kuwakamata wahusika wa tukio hilo kwa hatua zaidi za kisheria.

No comments: