Friday, February 3, 2017

DC MBINGA AWATAKA WADAU WA SHERIA KUTENDA HAKI NA KUTEKELEZA WAJIBU WAO IPASAVYO

Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa ucheleweshaji wa utoaji haki kwa wakati unasababisha kupoteza rasilimali muda na kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi, hivyo wito umetolewa kwa wadau wote washeria kuhakikisha kwamba wanatenda haki na kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

Aidha vitendo vya rushwa na kuweka vikwazo visivyokuwa na sababu ya msingi Mahakamani, ambavyo vinazuia utoaji wa dhamana kwa watuhumiwa vinachangia kuleta msongamano wa mahabusu gerezani.

Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye wakati alipokuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya sheria nchini yaliyofanyika kiwilaya katika viwanja vya Mahakama ya wilaya hiyo mjini hapa.

“Nasisitiza kwamba zile kesi ambazo zinauwezekano wa kutolewa dhamana zitolewe dhamana kwa wakati, tuache tabia ya kuwaweka mahabusu gerezani tupunguze wasiwepo wengi wanaokaa huko bila sababu yoyote ile ya msingi”, alisema Nshenye.


Alisema kuwa kuadhimisha siku ya sheria hapa nchini, kunaashiria kuanza rasmi kwa shughuli za kimahakama hivyo kauli mbiu ya umuhimu wa utoaji haki kwa wakati kuwezesha ukuaji wa uchumi, inapaswa kuzingatiwa kwa wadau wa sheria kufuata taratibu na sheria zilizowekwa bila kujenga ukandamizaji au ubaguzi katika jamii.

Naye kwa upande wake Hakimu mkazi wa Mahakama ya wilaya ya Mbinga, Magdalena Ntandu akitoa hotuba mbele ya wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo alisema kuwa upatikanaji wa haki kwa wakati kunasaidia jamii kujenga imani kwa vyombo vyote vya utoaji haki, kutambua na kuheshimu uwepo wa utawala wa sheria hapa nchini.

Ntandu alisema kuwa nchi yenye mfumo mzuri wa utawala wa sheria inatoa pia fursa sawa kwa wananchi wake mbele ya sheria na kujenga jamii yenye usawa, utulivu, ulinzi na amani.

“Na sio hivyo tu, hata pale haki inayotafutwa inapokuwa ni mojawapo ya rasilimali muhimu katika kuendeleza ama kukuza uchumi, haki hiyo ikicheleweshwa moja kwa moja inarudisha nyuma ukuaji wa uchumi wa mtu anayetafuta haki hiyo”, alisema.

Alibainisha kuwa wajibu wa Mahakama na wadau wengine katika utoaji haki kwa wakati, wanapaswa kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba mashauri yote yaliyofunguliwa inapofikia mwishoni mwa mwaka yawe yamemalizika ili unapoanza mwaka mwingine waweze kuanza na mashauri mapya.

Alifafanua kuwa kwa kutekeleza kauli mbiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli ya Hapa kazi tu, ina maana kwamba watu wote wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na kuepuka visingizio visivyokuwa vya lazima ambavyo vinakwamisha uadilifu na uwajibikaji ipasavyo katika jamii.

Pamoja na mambo mengine, awali naye Frank Kapinga akiwakilisha mawakili wenzake kwa kutoa hotuba katika sherehe hizo za maadhimisho ya siku ya sheria hapa nchini wilayani Mbinga, alifafanua kuwa zipo sababu nyingi zinazokwamisha utoaji haki kwa wakati huku akizitaja baadhi yake kuwa ni ukosefu wa miundombinu rafiki kwa utoaji haki, uhaba wa rasilimali watu, mbinu na kanuni za kisheria za ucheleweshaji zinazoletwa na wadau wa sheria wakiwemo serikali, mahakama, mawakili, na waendesha mashtaka.

Kapinga alisema kuwa Mahakama ikiwa ndiyo mhimili mkuu wa utoaji haki inao wajibu ambao imepewa kikatiba, inapaswa kusikiliza na kumaliza mashauri mbalimbali kwa muda unaostahili na kuondokana na tabia ya kuchelewesha kesi kwa kuziahirisha pasipo hata sababu zenye mashiko.

“Mahakama inalojukumu la kupambana na vitendo hivi vinavyokiuka maadili ya utendaji kazi hususani rushwa na jeuri ya madaraka ya kimahakama, inapaswa kuhakikisha wadau wote wanapata huduma stahili na ushirikiano ili waweze kutimiza majukumu yao ya kila siku kwa wakati”, alisisitiza Kapinga.

Hivyo basi aliongeza kuwa serikali inaowajibu pia wa kuhakikisha kwamba miundombinu ya mahakama na rasilimali watu vinaendana na mahitaji halisi ikiwemo huduma husika zinasogezwa karibu na wananchi, kama vile ujenzi wa Mahakama za mwanzo ambazo zipo chache na kusababisha wananchi kutembea umbali mrefu kufuata haki katika Mahakama hizo.

No comments: