Tuesday, February 7, 2017

MASHINDANO KUMTAFUTA BALOZI WA UTALII RUVUMA YAFANYIKA MAJIMAJI SONGEA

Samson Kahabuka, Mratibu wa kituo cha habari za utalii mkoa wa Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

MASHINDANO ya kumtafuta Balozi wa utalii mkoa wa Ruvuma, ambayo yanaratibiwa na Kituo cha habari za utalii mkoani humo yameanza kufanyika kwenye hoteli ya Majimaji iliyopo mjini Songea.

Mratibu wa kituo hicho, Samson Kahabuka alisema kuwa warembo 15 kutoka wilaya ya Songea wameanza mazoezi kwenye ukumbi wa hoteli hiyo ambapo lengo kuu la kufanya hivyo ni kuwapata warembo watakaotoka wilaya zote za mkoa huo.

Kahabuka alisema lengo kuu la shindano hilo ni kutangaza vivutio vyote vya mkoa wa Ruvuma, ambapo Februari 10 mwaka huu warembo 15 kutoka wilaya ya Songea watatembelea wilaya ya Nyasa ili kuweza kuona baadhi ya vivutio vya wilaya hiyo.


“Warembo hawa watakuwa Nyasa kwa siku mbili, wataona vivutio na kufanya tamasha majira ya usiku kwenye ukumbi wa Bay live ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa wilaya hiyo ya Nyasa’’, alisema Kahabuka. 

Vilevile alifafanua kuwa Februari 13 mwaka huu watapokelewa warembo kutoka wilaya nyingine, ili kuanza mazoezi rasmi ya kumsaka Balozi wa utalii yakishirikisha wilaya za Songea, Nyasa, Namtumbo, Tunduru na Mbinga yataanza kwenye hoteli hiyo ya Majimaji.

Pia alisema kuanzia wiki ya tatu ya mwezi Februari hadi Machi mwaka huu, warembo hao watafanya ziara ya kutembelea vivutio vya utalii ambavyo vipo mkoani hapa.

Mratibu huyo aliongeza kuwa fainali za kumpata Balozi huyo mkoani Ruvuma zinatarajiwa kufanyika Machi 31 mwaka huu mjini Songea.


Hata hivyo Kahabuka aliyataja baadhi ya manufaa ambayo mshiriki atayapata katika shindano hilo ni pamoja na kupata elimu ya mambo mtambuka ikiwemo elimu ya kujitambua, fursa ya ajira kwenye hoteli na kwamba kwa atakayeshinda atawakilisha mkoa huo ngazi ya kitaifa.

No comments: