Sunday, February 5, 2017

MBINGA WAENDELEA KUFANIKIWA ZOEZI LA UPIMAJI ARDHI

Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa hadi kufikia Disemba mwaka jana, mashamba yenye ukubwa wa ekari 78,149.065 sawa na hekta 31,259.626 yameingizwa na kupimwa katika mpango wa upimaji ardhi, ambapo halmashauri ya wilaya ya Mbinga katika kipindi hicho imefanikiwa kupima ekari 70,491.165 na ekari 7,657.9 zimepimwa kutoka halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma.

Kwa mujibu wa takwimu hizo na taarifa zilizomfikia mwandishi wetu kutoka vyanzo mbalimbali vya habari vimethibitisha kuwa, halmashauri hizo zinaendelea kutekeleza sheria za ardhi pamoja na kutimiza agizo la serikali la kupima kila kipande cha ardhi na kukimilikisha kwa walengwa husika.

Aidha halmashauri zimekuwa zikiendelea kuhamasisha wamiliki wa viwanja na mashamba kulipia kodi za ardhi pamoja na kuviendeleza viwanja vyao kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni pamoja na kusambaza hati za madai ya kodi kwa wadaiwa sugu na kwamba wale wanaoshindwa kulipa hufikishwa Mahakamani.


Vilevile kwa lengo la kuepuka migogoro ya ardhi katika upangaji, upimaji na ugawaji wa viwanja baina ya wamiliki wa ardhi na serikali wilaya ya Mbinga imekuwa ikitumia utaratibu wa upimaji shirikishi, bila kulipa fidia ambapo mmiliki wa ardhi huchangia gharama ya upimaji kwa kutoa asilimia 40 ya viwanja vitakavyopatikana katika ardhi yake.

Utoaji wa asilimia hiyo ya viwanja huenda kwa halmashauri kwa lengo la kufidia maeneo yote yatakayoangukia kwenye maeneo ya huduma za kijamii kama vile barabara, maeneo ya wazi, ujenzi wa zahanati, masoko na shule huku asilimia 60 ya viwanja itakayopatikana katika ardhi husika hubaki kwa mmiliki wa ardhi.

Pia kwa mwaka wa fedha 2016/2017 nayo halmashauri ya mji wa Mbinga, imeweza kufanikiwa kupima jumla ya viwanja 386 kwa kutumia utaratibu huo wa upimaji shirikishi.

Kadhalika mwandishi wa habari hizi amebaini pia kwa upande wa fidia wilaya hizo zimekuwa zikitumia mpango huo wa upimaji shirikishi ili kuepuka gharama za fidia na kwamba fidia husika hulipwa kwa mfumo wa utwaaji ardhi wa lazima kwa manufaa ya umma katika maeneo ambayo mpango huo hauwezi kutumika.

Halmashauri ya mji wa Mbinga inaendelea na jitihada za kujiongezea mapato ya ndani kwa kupima viwanja vya matumizi mbalimbali ambapo hadi kufikia Disemba mwaka jana, viwanja 55 vimepimwa katika eneo la uwanja wa ndege lililopo mjini hapa na kazi hiyo bado inaendelea.

Kwa mujibu wa nakala ya taarifa ya maendeleo ya wananchi ambayo nakala yake tunayo, inasisitiza kuwa mji huo unaendelea kufanya uthamini wa majengo ili kuwezesha kutoza kodi ya majengo (Property Tax) kulingana na thamani ya jengo husika.

Pamoja na mambo mengine kwa upande wa utatuzi wa migogoro mbalimbali ya ardhi wilaya ya Mbinga na halmashauri ya mji huo, imekuwa ikiendelea kupambana na utatuzi wa migogoro hiyo kwa kutenga siku moja ya Ijumaa ya kila mwisho wa mwezi na kuanzisha dawati la kupokea kero za wananchi zinazohusiana na masuala ya ardhi.

No comments: