Friday, February 3, 2017

WASHIKILIWA NA POLISI KWA TUHUMA YA KUJERUHI

Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linawashikilia wakazi wawili wanaoishi katika mtaa wa Pambazuko uliopo katika kata ya shule ya Tanga Manispaa ya Songea mkoani humo, kwa tuhuma ya kumjeruhi Abethi Ponera (25) kwa kumkata na kitu chenye ncha kali kwenye paja lake la mguu upande wa kulia na kumsababishia jeraha na maumivu makali.

Zubery Mwombeji.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Bernad Mng`ong`o (39) na Boniface Mbecha (27) wote wakazi wa mtaa huo.

Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 21 mwaka huu majira ya saa tano usiku, katika mtaa huo.

Alifafanua kwamba siku ya tukio hilo Ponera akiwa anarudi nyumbani kwake akitokea kunywa pombe kwenye kilabu cha pombe za kienyeji, ghafla alivamiwa na watu asiowafahamu na kuanza kumpiga kisha kumjeruhi paja lake la mguu wa kulia na kuathiri sehemu zake za siri.

Alisema kuwa Ponera kabla ya kukutwa na tukio hilo akiwa katika kilabu hicho ambacho kinamilikiwa na Mg’ong’o kulikuwa na malumbano kati yake na watu wengine aliokuwa anakunywa nao pombe hizo za kienyeji, ambao walikuwa wakimtaka ifikapo Januari 22 mwaka huu aende kwenye uchaguzi mdogo akamchague mgombea udiwani wanayemtaka wao (chama ambacho jina lake linahifadhiwa) jambo ambalo Ponera alipingana nalo kisha baadaye aliamua kuondoka kuelekea nyumbani.


Alieleza zaidi kuwa askari Polisi waliokuwa doria siku hiyo walimkuta Ponera akiwa njiani amelala huku damu zikimtoka kutokana na jeraha kubwa alilokuwa nalo.

Vilevile aliongeza kuwa askari hao walimchukua na kwenda naye hadi kituo kikuu cha Polisi ambako alipatiwa hati ya matibabu na baadaye alipelekwa hospitali ya Rufaa Songea ambako amelazwa akiendelea kupatiwa matibabu.


Pia Kamanda Mwombeji alieleza kuwa uchunguzi wa awali umebaini kwamba kabla ya Ponera kujeruhiwa kutokana na kuwa katika kilabu hicho mmiliki wa kilabu hicho, Mg’ong’o na mwenzake Mbecha waliwakamata kwa mahojiano zaidi na upelelezi utakapokamilika watafikishwa Mahakamani.

No comments: