Monday, January 30, 2017

WANAFUNZI CHUO CHA MAAFISA TABIBU SONGEA WAISHI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU WAITUPIA LAWAMA SERIKALI

Waziri wa afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto, Ummy Mwalimu. 
Na Kassian Nyandindi,       
Songea.

WANAFUNZI wanaosoma katika chuo cha Maafisa tabibu Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wameilalamikia serikali kwa kitendo cha kusitisha huduma ya kutoa chakula chuoni hapo jambo ambalo linawafanya baadhi yao kushindwa kumudu gharama za kununua chakula hicho na kuwafanya waishi maisha magumu.

Aidha kufuatia hali hiyo uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini pia wanafunzi wa kike, baada ya muda wa masomo hujiuza kimwili mitaani kwa kufanya mapenzi ili waweze kupata fedha za kujikimu ikiwemo kununua chakula na kuendesha maisha yao.

Kadhalika wanafunzi hao wapo hatarini kuambukizwa na magonjwa kutokana na mazingira ya chuo hicho, ikiwemo vyoo na mabafu ya kuogea wanafunzi kuwa katika hali mbaya.

Vilevile majengo yanayotumika kulala wanafunzi hao nayo yamekuwa chakavu kutokana na serikali, kutoyafanyia ukarabati kwa miaka mingi na kusababisha adha kubwa kwa watumiaji wa miundombinu ya chuo hicho.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi mjini hapa, wanafunzi hao walisema kuwa chuoni hapo miaka miwili iliyopita serikali ilikuwa ikisambaza chakula kupitia wazabuni, lakini huduma hiyo imesitishwa ghafla na sasa wanalazimika kuchangishana fedha kila mwezi ili waweze kupata chakula.

“Kwa upande wa huduma ya umeme na maji tumekuwa pia tukichangishana fedha kulipia gharama husika ili tuweze kuishi na kuendesha masomo hapa chuoni, tunaiomba serikali itatue matatizo haya tuliyonayo kwani yanatufanya tuwe katika hali ngumu kimaisha”, walisema.

Akihojiwa na mwandishi wetu ofisini kwake, Mkuu wa chuo hicho Dkt. Salustian Salla alikiri kuwepo kwa changamoto hizo na kueleza kuwa majengo ya chuo hicho cha maafisa tabibu tangu yajengwe mwaka 1974, yamefanyiwa ukarabati mara moja tu kipindi cha utawala wa Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa.

Dkt. Salla alisema kuwa chuo hicho ambacho kinamilikiwa na Wizara ya afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wanafahamu juu ya changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo uchakavu wa majengo hayo.

“Hili la wanafunzi kujiuza kwa kweli sijawahi kusikia, lakini tumekuwa na changamoto nyingi miundombinu yetu haifai kwa matumizi ya binadamu hivyo wakati mwingine tumekuwa tukilazimika kutumia ada za wanafunzi kukarabati vyoo ambavyo sakafu zake hubomoka”, alisema Dkt. Salla.

Aliongeza kuwa changamoto nyingine wanayokabiliana nayo ni ukosefu wa walimu wa kufundisha darasani ambapo mpaka sasa, chuo kina walimu wawili tu na kwamba wakati mwingine hulazimika kuomba madaktari wanaotoka nje ya chuo hicho kwa ajili ya kufundisha wanafunzi hao.

Alibainisha kuwa fedha za uchangiaji wa gharama za masomo ambazo wanafunzi huchangia, ndiyo wakati mwingine hutumika kumlipa posho mwalimu anayetoka nje ya chuo hicho ambaye hujitolea kwenda kufundisha.

Pamoja na mambo mengine, akizungumzia juu ya huduma ya chakula chuoni hapo alifafanua kuwa katika kipindi cha nyuma serikali ilikuwa inaleta fedha kwa ajili ya kununua chakula cha wanafunzi na kwamba wamesimamisha kutoa huduma hiyo kutokana na sababu ya kushindwa kulipa wazabuni.

“Kama unavyoona mazingira ya chuo chetu, hatuna hata uzio kuzunguka chuo hiki watu wamekuwa wakiingia katika maeneo ya chuo bila kufuata utaratibu kwani hata usalama wa mazingira yetu ni mdogo”, alisema.


Hata hivyo alisema ni miaka miwili sasa imepita tokea serikali isitishe huduma ya wazabuni kusambaza chakula kwa wanafunzi wa chuo cha maafisa tabibu katika Manispaa ya Songea na mpaka sasa bado hawajalipwa fedha zao kwa kazi waliyofanya ya kusambaza chakula hicho.

No comments: