Sunday, January 1, 2017

CCM YAPANIA KUCHUKUA USHINDI UCHAGUZI MDOGO KATA YA MAGUU MBINGA

Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma kimewataka wananchi wa kata ya Maguu wilayani Mbinga mkoani hapa, kumchagua mgombea anayetokana na chama hicho katika uchaguzi wa nafasi ya udiwani unaotarajiwa kufanyika Januari 22 mwa huu.

Akizungumza juzi na wananchi wa kata hiyo katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani zilizofanyika katika viwanja vya michezo mji mdogo wa Maguu Mwenyekiti wa CCM wa mkoa hu, Oddo Mwisho alisema kuwa wanachama na wananchi kwa ujumla wake wanapaswa kukiamini chama hicho kwa kuwa ndicho pekee chenye nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Mwisho alisema kata hiyo ilikuwa mikononi mwa CCM hivyo wananchi wanakila  sababu ya kuendelea kukiamini na kwamba vyama vya upinzani havipaswi kupewa kuongoza kata hiyo kutokana na kukosa historia ya kuwatumikia wananchi ipasavyo katika kuwaletea maendeleo kwenye maeneo yao wanayoishi.


“Ndugu zangu wananchi kumbukeni jinsi ambavyo majimbo na kata ambazo vyama vya upinzani wamepata nafasi ya kuongoza wameshindwa kuwaletea maendeleo, kila kukicha wao kazi yao kubwa ni kuhamasisha maandamano ya kupinga mambo ambayo yanatekelezwa na serikali ya chama tawala”, alisema.

Alisema halmashauri ya wilaya ya Mbinga inaundwa na madiwani wa kutoka katika kata 28 wanatokana na CCM hivyo kinachotakiwa kwa wananchi wa Maguu ni kuhakikisha wanamchagua mgombea wa chama hicho tawala, ili akaungane na wenzake katika kuwakilisha matatizo yao kwenye vikao vya baraza la madiwani.

Mwisho alisisitiza juu ya umuhimu wa kuondoa mifarakano miongoni mwa wanachama wake jambo ambalo litarahisisha upatikanaji wa ushindi katika uchaguzi huo na kwamba, kwa wale ambao wataonekana kukisaliti chama hakitasita kuwachukulia hatua.

Kwa upande wake mgombea Manfred Kahobela akiomba ridhaa kwa wanachama wake na wananchi wakati wa uzinduzi huo alisema kuwa, endapo kama atachaguliwa atahakikisha anatekeleza majukumu yake ya kujenga ushirikiano nao katika kufanya shughuli za maendeleo na kwamba zile ahadi zilizoachwa na mtangulizi wake atazipatia kipaumbele na sio vinginevyo.

Kahobela alisema anafahamu changamoto mbalimbali ambazo wananchi wa kata hiyo wanakabiliana nazo hivyo kinachotakiwa sasa wananchi ambao ni wapiga kura katika kata hiyo, wahakikishe ifikapo Januari 22 mwa huu wanamchagua ili aweze kuzipatia ufumbuzi wa kudumu katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.


Uchaguzi huo mdogo unafanyika kufuatia diwani wa kata hiyo ya Maguu Nathaniel Hyera kufariki dunia kutokana na kuugua ugonjwa wa shinikizo la damu, ambapo alifikwa na mauti Marchi 8 mwaka jana wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya Mbinga mkoani hapa.

No comments: