Monday, January 30, 2017

KAYA MASKINI SONGEA WAKATA RUFAA TASAF MAKAO MAKUU

Na Mwandishi wetu,    
Songea.

KAYA masikini 260 kati ya kaya 2,692 zilizoenguliwa katika Mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wa kunusuru kaya maskini, katika Manispaa ya Songea mkoani hapa zimeandika barua kupeleka Ofisi za TASAF makao makuu jijini Dar es Salaaam, kwa lengo la kukata rufaa juu ya kuenguliwa kwao.

Ofisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema kaya hizo 2,692 kati ya kaya 7,695 zilizokuwa zinanufaika na ruzuku hiyo zimeenguliwa baada ya uhakiki wa nyumba kwa nyumba uliofanyika mwaka jana, ambapo baada ya uhakiki huo kaya zenye sifa zilibakia 5,003.

Midelo alieleza kuwa kati ya kaya zilizoenguliwa ilibainika kuwa kaya 1,599 katika Manispaa ya Songea sio masikini, kaya 342 walihama katika maeneo yao, kaya 110 walifariki, kaya 417 zilibainika kuwa ni hewa na kaya 144 hazikuwepo kwenye uhakiki huo.

Alisema kuwa mara baada ya kaya zilizoenguliwa kupata barua ya kuondolewa kwao, yametokea malalamiko mengi katika kaya hizo hali ambayo imesababisha Manispaa ya Songea kupita katika mitaa ya walioenguliwa na kutoa elimu ya kukata rufaa kwa wale wanaodhani wameonewa na wale ambao wametolewa kwa uhalali kuanza kulipa.


Kaimu Mratibu wa TASAF Manispaa ya Songea, Mensa Ngerangera akitoa elimu kwa nyakati tofauti katika mitaa ya Ruhuwiko kanisani, Ruhuwiko shuleni, Namanditi, Lilambo A na Sinai amewataka wale wote ambao wametolewa kwa kukosa sifa waanze kulipa kama vile ilivyoelekezwa kwenye barua.

Ngerangera alieleza kuwa kaya maskini ambazo zimeondolewa kimakosa katika mpango huo zinatakiwa kukata rufaa kwa kuandika barua TASAF makao makuu na kwamba ambaye hataandika barua ya rufaa atatakiwa kuanza kulipa deni hilo.

Amezitaja sifa za kaya zinazotakiwa kukata rufaa kuwa ni zile ambazo zinakula mlo mmoja kwa siku, kaya isiwe na zaidi ya heka moja, asiwe mfanyabiashara, mstaafu wala mwenye mtoto au ndugu wa karibu ambaye ni mtumishi wa umma na asiwe mwenye nyumba bora iliyoezekwa kwa bati na  kupiga sakafu.

Utafiti ambao umefanywa katika baadhi ya mitaa ambayo wameenguliwa waliokuwa wanufaika, umebaini kuwa kuna kaya ambazo zimeondolewa kwa makosa kwa kuwa zina sifa ya kaya maskini, ingawa pia zipo kaya ambazo hazina sifa ya kaya maskini hivyo wanastahili kuenguliwa.

Ngerangera alisema Novemba hadi Disemba mwaka jana kiasi cha shilingi milioni 277 zimetolewa kwa kaya maskini ambazo zina sifa, katika mitaa 53 ya Manispaa ya Songea ambapo Januari hadi Februari mwaka huu 2017 Manispaa hiyo itatoa kiasi cha shilingi milioni 256 kwa kaya maskini zenye sifa.

No comments: