Sunday, January 1, 2017

MANISPAA SONGEA YATOA MKOPO MILIONI 72.5 KWA VIKUNDI VYA UJASIRIAMALI

Tina Sekambo Mkurugenzi Manispaa ya Songea.
Na Kassian Nyandindi,      
Songea.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imetoa mkopo wa shilingi milioni 72.5 ambazo zimetokana na mapato yake ya ndani kwenda katika vikundi vya wanawake na vijana ili waweze kujikomboa kiuchumi.

Mkopo huo umetolewa katika kipindi cha mwaka jana kwa awamu mbili ambapo katika awamu ya kwanza jumla ya shilingi milioni 52.5 zilikopeshwa kwenye vikundi hivyo.

Aidha kati ya fedha hizo vikundi 73 vya wanawake vilikopeshwa zaidi ya shilingi milioni 36 na vikundi 35 vya vijana vilikopeshwa shilingi milioni 16.


Kwa mujibu wa Ofisa habari wa Manispaa ya Songea, Albano Midelo alisema kuwa katika awamu ya pili Manispaa imetoa mkopo wa shilingi milioni 20 kwa vikundi ambapo vikundi vya wanawake 32 vilipewa shilingi milioni 15.4 na vikundi 10 shilingi milioni 4.6.

Alisema vikundi hivyo vimetoka katika kata 21 zilizopo katika Manispaa hiyo na kwamba mikopo iliyotolewa ni kati ya shilingi laki sita hadi nane kwa kila kikundi ambazo wanatakiwa kurejesha baada ya miezi 12 ili waweze kukopeshwa wengine kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao za ujasiriamali.

Kwa ujumla Manispaa ya Songea imekuwa ikitoa mikopo hiyo kwa riba ya asilimia kumi tu kwa kipindi cha mwaka mmoja, ambapo asasi nyingi za kifedha zimekuwa zikitoa riba kubwa yenye makato mengi hali inayosababisha wakopaji wengi wenye kipato kidogo kushindwa kufikia malengo yao.


Mkopo huo unatolewa kwa vikundi vya wajasiriamali vya wanawake na vijana kwa sheria ya Bunge ya mwaka 1993 ambayo imeagiza kutoa mkopo kwa kutumia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri husika, lengo ikiwa ni kuinua hali ya uchumi katika makundi hayo mawili.

No comments: