Sunday, January 22, 2017

BREAKING NEWS: WAJUMBE WA BODI MBINGA KURUGENZI SACCOS WASWEKWA RUMANDE KWA TUHUMA YA WIZI WA MAMILIONI YA FEDHA

Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

WATUMISHI saba wanaotoka katika Halmashauri ya mji wa Mbinga, wilaya ya Mbinga na Nyasa mkoani Ruvuma ambao pia ni Wajumbe wa bodi ya Chama cha ushirika Mbinga Kurugenzi SACCOS iliyopo mkoani hapa, wamekamatwa na kuwekwa mahabusu wakituhumiwa kuiba shilingi milioni 405,204,514 za wanachama wa chama hicho na kusababisha hasara kubwa kwa SACCOS hiyo kushindwa kujiendesha kwa manufaa ya wanachama.

Cosmas Nshenye Mkuu wa wilaya ya Mbinga.
Aidha hatua hiyo ya kukamatwa kwa Wajumbe hao ilitolewa na Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani humo, Biezery Malila baada ya kusomwa taarifa ya ukaguzi juu ya mwenendo wa chama hicho cha ushirika ambayo ilibainisha wizi wa fedha hizo katika mkutano mkuu maalumu wa wanachama, uliofanyika Januari 21 mwaka huu kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.

“Kwa masikitiko makubwa ndugu zangu naomba niwaeleze kwamba mwenendo wa chama hiki sio mzuri kwa kuwa wajumbe wa bodi hii wameshiriki kwa namna moja au nyingine kukiuka taratibu za uendeshaji wa chama hiki, hivyo wanapaswa kuwajibika kwa mujibu wa sheria na taratibu husika za vifungu vya uendeshaji wa vyama vya ushirika”, alisema Malila.

Mrajisi huyo wa vyama vya ushirika mkoa wa Ruvuma alifafanua kuwa fedha hizo ambazo wajumbe hao wanadaiwa kujinufaisha kwa matakwa yao binafsi zilitokana na mkopo wa shilingi milioni 500 uliotolewa na benki ya CRDB kwa ajili ya kukopeshwa wanachama lakini cha kushangaza waliamua kuzitumia kinyume na taratibu husika.

Pia alimtaja mtuhumiwa mwingine wa nane ambaye sio mtumishi wa serikali na ni Meneja wa SACCOS hiyo kuwa ni, Raymond Mhagama ambapo ametoroka kufuatia kuwepo kwa kesi ya ubadhirifu wa fedha hizo na kwamba madai yake ya kutoroka huko yamefunguliwa Kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga na kwamba, anatafutwa popote pale alipo ili aweze kukamatwa na kujibu tuhuma hizo zinazomkabili mbele yake.


Malila aliongeza kuwa fedha hizo ambazo zililenga kuwakopesha wanachama wa Mbinga Kurugenzi SACCOS, Wajumbe hao wamejinufaisha kwa matakwa yao binafsi hivyo wanatakiwa kulipa kwa mujibu wa kifungu namba 55 cha sheria ndogo namba 13 ya ushirika namba 6 ya mwaka 2013.

Kadhalika kufuatia kuwepo kwa tukio hilo Mrajisi huyo ametoa wito kwa viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika mkoa wa Ruvuma, kuanzia sasa amewaonya kuacha vitendo vya wizi wa fedha na mali za ushirika na kwamba Ofisi ya Mrajisi msaidizi mkoani humo inaendelea kuchukua hatua za kuwafungulia mashtaka wale wote watakaobainika kushiriki katika upotevu wa mali za ushirika.

Vilevile Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji amewataja watumishi hao saba waliowekwa mahabusu mpaka sasa kuwa ni Zackaria Lingowe, Emmanuel Mwasaga na Alex Kalilo ambao ni watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Nyasa, Jamima Challe na Stella Mhagama wanatoka halmashauri ya mji wa Mbinga, Lucas Nchimbi na Mhadisa Meshack nao ni watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga na kwamba mpaka sasa bado wanashikiliwa na Jeshi la Polisi wakiendelea kuhojiwa kutokana na tuhuma zinazowakabili.

Awali wakichangia hoja kwa nyakati tofauti katika mkutano huo wanachama wa SACCOS hiyo waliunga mkono jitihada hizo zilizochukuliwa na Mrajisi huyo wa vyama vya ushirika mkoani hapa, huku wengine wakidai kuwa wamesikitishwa kwa taarifa hizo ambazo ni utovu mkubwa wa nidhamu uliofanyika ndani ya chama chao juu ya matumizi mabaya ya fedha za wanachama.

Batson Mpogolo ambaye ni mmoja kati ya wanachama wa ushirika huo alisema kuwa taarifa hiyo ya mkaguzi ambayo imesomwa mbele yao inaonesha kuwa na madudu mengi ya ubadhirifu wa fedha na dosari za kiutendaji, hivyo kwa uchungu walionao wanachama kuna kila sababu kwa viongozi wao kuchukuliwa hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.

Pamoja na mambo mengine chama hicho cha ushirika kinaundwa na wanachama ambao ni watumishi wa serikali kutoka katika halmashauri ya mji wa Mbinga, wilaya ya Mbinga na Nyasa ambapo makao makuu ya Ofisi zake yapo Mbinga mjini.

Hata hivyo katika mkutano huo hatua iliyofuata ilikuwa ni ya kuvunja bodi ya Chama hicho cha ushirika Mbinga Kurugenzi SACCOS kufuatia kuwepo kwa matatizo hayo ya wizi wa fedha za wanachama na kwamba uchaguzi wa kuteua Wajumbe wengine wa bodi hiyo utafanyika Januari 31 mwaka huu.

No comments: