Wednesday, January 4, 2017

MAJALIWA APONGEZA KUKUA KWA PATO LA MWANANCHI WA KAWAIDA RUVUMA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipunga mkono leo katika uwanja wa ndege Songea mjini mara baada ya kuwasili kwa ajili ya kuanza ziara ya kikazi ya siku tano mkoani Ruvuma, kulia ni mkewe mama Mary Majaliwa, kulia kwake ni Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge na Mkuu wa wilaya ya Songea Palolet Mgema.
Na Kassian Nyandindi,           
Songea.

PATO la Mwananchi wa kawaida hapa nchini (Percapital income) katika mkoa wa Ruvuma limepanda kutoka shilingi milioni 2,082,167 mwaka juzi hadi kufikia shilingi milioni 2,415,485 kwa mwaka 2016, hatua ambayo imeufanya mkoa huo kushika nafasi ya tatu kitaifa ikitanguliwa na mikoa ya Dar es Salaam na Iringa.

Aidha pato hilo linaonesha kwamba ni ongezeko la asilimia 16 ikilinganishwa na pato la mtu mmoja kwa mwaka 2014  ambapo ongezeko hilo limetokana na shughuli ya kiuchumi kama vile kilimo ambacho hutegemea kwa kiasi kikubwa wakazi wa mkoa huo kuendeshea maisha yao.

Hayo yalisemwa leo na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya mkoa huo kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Ikulu ndogo mjini Songea.

Dkt. Mahenge alisema kuwa wananchi wake hutegemea shughuli hizo kiuchumi ambapo zaidi ya asilimia 87 ya wakazi wake, hupata riziki yao kutokana na shughuli hiyo ambayo huchangia pia pato la taifa kwa asilimia 3.3 kwa mwaka, huku pato la mkoa likifikia wastani wa asilimia 75.


Alifafanua kuwa mkoa wa Ruvuma, unafursa nyingi ambazo hutumiwa katika kusukuma mbele maendeleo ya mkoa ambapo eneo kubwa la mkoa huo linafaa kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji na kuufanya mkoa kuwa ni miongoni mwa mikoa michache yenye bahati ya kupata mvua za kutosha ambazo hunyesha kuanzia mwezi Novemba hadi Mei kila mwaka.

Mkuu huyo wa mkoa alielezea kuwa kufunguka pia kwa miundombinu ya barabara inayounganisha makao makuu ya mkoa na wilaya zake, pamoja na mikoa mingine imesaidia kwa kiasi kikubwa kuharakisha kukua kwa shughuli za kiuchumi katika mkoa wa Ruvuma.

Alisema kuwa malengo ya kilimo katika msimu wa mwaka 2015/2016 mkoa ulilenga kulima jumla ya hekta 892,525 za mazao ya chakula na biashara zilizotarajiwa kutoa mavuno tani 2,377,004 ambapo mazao ya chakula ilitarajiwa kulimwa hekta 637,663 zilizotarajiwa kutoa mavuno tani 1,939,946 na mazao ya biashara ilitarajiwa kulimwa hekta 254,862  na kutoa  mavuno tani 437,058.

Vilevile utekelezaji wa malengo hayo hadi kufikia mwezi Juni mwaka jana, mkoa huo ulikwisha zalisha hekta 877,035 sawa na asilimia 98.3 ya lengo lililowekwa ambalo lilikuwa ni kuzalisha jumla ya hekta 892,525 zilizotoa mavuno tani 2,127,180 sawa na asilimia 89.4.

Pia alibainisha kuwa kati ya hekta hizo za kilimo cha mazao ya chakula jumla zililimwa hekta 703,709 ambazo zimetoa mavuno ya tani 1,955,424 na kwamba katika kilimo cha mazao ya biashara hekta zilizolimwa ni 173,326 na zilitoa jumla ya hekta 171,756 za mavuno yote.

Kwa upande wake Waziri Mkuu, Majaliwa alipongeza jitihada hizo zinazofanywa na viongozi wa mkoa wa Ruvuma ikiwemo kukua kwa pato hilo la mwananchi wa kawaida, huku akisisitiza kuwa zisiishie hapo wanachopaswa ni kuendelea kuhamasisha wananchi wazalishe mazao ya chakula na biashara kwa wingi ili waweze kuondokana na umaskini. 


No comments: