Thursday, January 5, 2017

MAJALIWA AZIAGIZA HALMASHAURI NCHINI KUTAMBUA VYANZO VYA MAJI NA KUHIFADHI VISIHARIBIWE

Wananchi wa kijiji cha Magingo na Mkongotema wakimlaki Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa baada ya kuwasili katika kijiji hicho kufungua mradi mkubwa wa maji uliogharimu shilingi bilioni 1.9 ambao utahudumia wananchi wa vijiji hivyo viwili.
Na Kassian Nyandindi,          
Songea.

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameagiza Halmashauri zote za wilaya hapa nchini zitambue vyanzo vyote vya maji na hatimaye vitunzwe na kuhifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

Aidha Majaliwa amesema kuwa nia ya serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata maji safi na salama, hivyo hawana budi kuwa na tabia ya kutunza vyanzo hivyo kwa manufaa ya jamii.

Majaliwa alisema hayo leo wakati alipokuwa akifungua mradi wa maji wa vijiji vya Mkongotema na Magingo wilaya ya Songea vijijini mkoani Ruvuma, ambao ujenzi wake umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.9 na wenye uwezo wa kuhudumia wakazi 5,300 wanaoishi katika maeneo hayo.


Alisema kuwa ili mradi huo uweze kuwa endelevu wananchi katika maeneo mengine ambako miradi kama hiyo inatekelezwa, wanapaswa kujenga tabia ya kuchangia miradi yao ya maendeleo hasa pale inapojengwa ili iweze kukamilika kwa wakati.

“Maeneo ambayo wananchi wamekuwa hawachangii miradi ya maendeleo huwa inakwama ujenzi wake na haikamiliki kwa wakati na ili miradi hii, iweze kudumu kwa muda mrefu wananchi wanapaswa kujenga tabia ya kutunza vyanzo vya maji”, alisisitiza Majaliwa.

Pia alieleza kuwa wananchi waache tabia ya kuchoma moto hovyo, kukata miti, kulima na kuingiza mifugo karibu na vyanzo hivyo badala yake wapande miti rafiki ya maji kwa wingi ili kuweza kutunza uoto wake wa asili.


Katika kufanikiwa hilo, amesisitiza juu ya umuhimu wa uundwaji wa kamati za maji vijijini ambazo zitakuwa na wajibu wa kusimamia vyanzo vya maji na miundombinu mingine ya maji katika eneo husika ikiwemo kuhakikisha kwamba matumizi ya maji yanakuwa sahihi wakati wote.

No comments: