Saturday, January 21, 2017

SONGEA WAIOMBA WIZARA KUWAPELEKEA WALIMU MASOMO YA SAYANSI

Na Kassian Nyandindi,   
Songea.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, inakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati katika shule za sekondari jambo ambalo linarudisha nyuma, maendeleo ya mkoa huo kwa watoto wanaopenda kusoma masomo hayo.

Aidha imeelezwa kuwa mahitaji ya walimu wa masomo ya sayansi katika Manispaa hiyo ni walimu 375 ambapo waliopo sasa ni 132 tu, hivyo kuwa na upungufu wa walimu 243.

Ofisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo amewaeleza waandishi wa habari kuwa Manispaa ina ziada ya walimu 192 wa masomo ya sanaa, katika shule za sekondari ambapo mahitaji ya walimu katika masomo hayo ni 536 wakati walimu waliopo ni 728.


Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa katika shule za sekondari 24 za serikali zilizopo katika Manispaa ya Songea zina jumla ya walimu 856 wanaofundisha masomo ya sayansi na sanaa.

Kwa mujibu wa Ofisa habari huyo anafafanua kwamba pia katika shule za msingi 76 za serikali zenye jumla ya wanafunzi 50,119 wakiwemo wavulana 24,656 na wasichana 25,463 zina upungufu wa walimu 95 wa masomo mbalimbali.


Hata hivyo aliitaja mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo, kuwa Manispaa hiyo imeomba Wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi kutoa kipaumbele kwa mikoa ya pembezoni kuwapangia idadi kubwa ya walimu wa sayansi badala ya kupangiwa walimu wa masomo ya historia, kiswahili na jiografia ili kuweza kuziba pengo hilo.

No comments: