Tuesday, January 3, 2017

WAZIRI MKUU KUANZA ZIARA YAKE YA KIKAZI KESHO MKOANI RUVUMA

Na Mwandishi wetu,      
Songea.

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kesho anatarajia kuanza ziara yake ya kikazi ya siku tano mkoani Ruvuma ambapo atapata fursa ya kutembelea na kukagua shughuli za maendeleo ya wananchi, katika wilaya ya Mbinga na Songea mkoani hapa.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa mkoa huo, Dkt. Binilith Mahenge alisema kwamba Majaliwa atawasili katika uwanja wa ndege Songea majira ya saa 9.00 alasiri na kupokelewa na viongozi wa serikali na chama.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Aliwataka wananchi wote kwenye maeneo ambayo Waziri huyo atafanya mikutano, wahudhurie kwa wingi ili kumsikiliza na hatimaye kutekeleza maagizo yake ambayo atayatoa kwa viongozi, watendaji na wananchi kupitia mikutano hiyo.

Dkt. Mahenge alisema kuwa mara baada ya kuwasili ataelekea Ikulu ndogo iliyopo mjini hapa, ambako atapokea taarifa ya maendeleo ya mkoa na kwamba baada ya hapo atazungumza na watumishi wa umma.

Alisema kuwa Januari 5 mwaka huu Waziri mkuu atatembelea katika halmashauri ya Songea vijijini Madaba ambapo atazungumza pia na watumishi wa serikali, kukagua na kuzindua mradi wa maji katika kijiji cha Magingo na baadaye atahutubia mkutano wa hadhara wananchi wa Madaba.


Dkt. Mahenge alifafanua kuwa Januari 6 mwaka huu, Majaliwa atatembelea na kukagua shughuli za uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe kwenye mgodi wa Ngaka uliopo katika kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga.

Alisema kuwa atakapokuwa kwenye kata hiyo atazungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara na kwamba Januari 8 mwaka huu atahitimisha ziara yake kwa kufanya kikao cha majumuisho Ikulu ndogo mjini Songea na kurejea jijini Dar es salaam.

Wakati huo huo Mkuu huyo wa mkoa amewataka wananchi wa mkoa wa Ruvuma kuhakikisha kwamba wanapanda kwa wingi mazao yanayostahimili ukame kutokana na kutonyesha mvua ya kutosha kama ilivyozoeleka miaka ya nyuma, na kwamba wajiwekee chakula cha kutosha ili waweze kukabiliana na uwezekano wa kutokea njaa.


Pia Dkt. Mahenge alisisitiza juu ya umuhimu wa kutunza mazingira kwa kuacha kukata na kuchoma moto misitu au kuchoma mkaa jambo ambalo limekuwa likisababisha kutokea kwa mabadiliko ya tabia nchi, kama Afrika na dunia kwa ujumla wake.

No comments: