Saturday, January 28, 2017

MKUU WA MKOA RUVUMA ACHUKIZWA NA UTENDAJI KAZI WA TFS SONGEA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge akikagua mradi wa uoteshaji miti unaosimamiwa na Wakala wa misitu Tanzania (TFS) wilaya ya Songea mkoani humo.
Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

UONGOZI wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wilaya ya Songea mkoani Ruvuma umetakiwa kuhakikisha kwamba, unasimamia vyema rasilimali zitokanazo na misitu ili ziweze kuwanufaisha Watanzania wote badala ya kujinufaisha watu wachache.

Aidha maofisa ardhi, maliasili na mazingira wilayani humo wanapaswa kujitathimini upya katika utendaji wa kazi zao za kila siku kwani kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya uwepo wa vitendo vya rushwa katika ofisi zao wilayani hapa.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge alisema hayo juzi mjini hapa akimtaka Ofisa misitu wilayani Songea, Godfrey Luhimbo kumaliza kero hizo haraka kabla serikali haijachukua hatua kali dhidi yake.

Dkt. Mahenge alisema kuwa serikali haitaki ubabaishaji katika usimamizi wa rasilimali zake kwani inataka kuona namna gani rasilimali hizo zinavyowanufaisha wananchi, ambapo amemtaka kuwa makini katika usimamizi na utoaji wa vibali vya misitu hasa baada ya kupata taarifa kwamba vibali hivyo hutolewa kinyume na taratibu za serikali kwa watendaji hao kuendekeza vitendo vichafu vya rushwa.


“Nakupa masaa matatu kuanzia sasa nahitaji taarifa sahihi ya namna unavyotoa vibali vya uvunaji wa mazao ya misitu, nimepata taarifa wewe unatoa vibali kwa njia ya rushwa na umekuwa ukipeleka siku mbele za kuwaandikia waombaji vibali hivyo ambavyo vipo katika mfumo sahihi unaokubalika kisheria”, alisema Dkt. Mahenge.

Alisema kuwa mtumishi wa umma unapopewa jukumu la kiutendaji ni lazima kutekeleza kwa misingi ya haki, usawa na sheria, kwani kinyume na hapo serikali haitakuwa tayari kuendelea kufanya kazi na mtumishi wa aina hiyo ambaye anailetea serikali hasara kubwa.

“Wewe ni mkuu wa idara umekuwa ukitoa vibali vya mdomo badala ya maandishi, jambo hili linaashiria kuhusika moja kwa moja na vitendo vya rushwa ipo siku tutakukamata na kukufikisha katika vyombo vya sheria, taarifa niliyonayo Ofisini kwangu mchango wa idara yako kiuchumi ni mdogo wewe unatumia ofisi ya umma kwa kujinufaisha wewe binafsi”, alisema.

Kufuatia hali hiyo amemuagiza Mkuu wa wilaya ya Songea, Palolet Mgema kuhakikisha kwamba anasimamia vizuri utekelezaji wa rasilimali za misitu katika wilaya hiyo, kwa kila alichoeleza kuwa imebainika kwamba kuna baadhi ya watumishi wa idara hiyo ni mizigo ambapo wanafanya kazi kwa mazoea na hawana mchango kwa taifa hili.

Sambamba na hilo amewataka kulipatia umuhimu suala la usimamizi wa misitu na utoaji vibali halali kwa wafanyabiashara kwa sababu wapo baadhi yao wanavuna magogo ya miti hupasua mbao na wengine kuchoma mkaa bila kibali kilichotolewa na serikali.

Katika hatua nyingine Dkt. Mahenge ameziagiza halmashauri zote nane zilizopo mkoani Ruvuma, kuweka alama zinazoonesha mipaka na maeneo ambayo hayaruhusiwi kufanyika shughuli za kibinadamu kama vile kilimo ili kuweza kulinda vyanzo vya maji na uhifadhi wa mazingira.

Vilevile kwa upande wake Meneja wa Wakala wa huduma za misitu wilaya ya Songea, Manyise Mpokigwa ameiomba serikali kuona umuhimu wa kusaidia katika suala zima la ulinzi wa misitu hiyo kwani kasi ya uchomaji moto na mkaa imekuwa kubwa jambo ambalo linaharibu uhai wa misitu hiyo ikiwemo uoto wake wa asili.


Mpokigwa alisema bado TFS inaendelea na kazi ya upandaji miti katika maeneo mbalimbali kama vile Wino, Mahanje pamoja na kugawa mbegu za miti kwa wananchi ambao wanaendelea kupanda katika maeneo yao.

No comments: