Sunday, January 22, 2017

WAKAZI MANISPAA SONGEA WATAKA MKANDARASI AMALIZE UJENZI WA BARABARA KWA WAKATI ULIOPANGWA

Na Mwandishi wetu,     
Songea.

BAADHI ya wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wameuomba uongozi wa Manispaa hiyo kumuhimiza Mkandarasi wa kampuni ya Lukoro Construction Limited, ambayo imepewa kazi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami mjini hapa kukamilisha ujenzi huo kwa wakati uliopangwa.

Wakizungumza na waandishi wa habari mjini hapa wakazi wa maeneo ya Matarawe, Bombambili, Mateka na Matogoro walisema kuwa licha ya kuwa kazi hiyo inayofanywa na mkandarasi huyo inaendelea kufanyika, lakini bado jitihada zinahitajika kuona namna ya kumaliza ujenzi huo mapema wakidai kuwa mvua zitakapoanza kunyesha kwa wingi zinaweza kusababisha kuchelewa kukamilisha ujenzi huo.

Amina Komba mkazi wa eneo la Matarawe alisema kuwa Kampuni ya ukandarasi ya Lukoro kwa muda mrefu ilianza kutengeneza barabara ya kutoka Bombambili hadi Mwembechai, lakini mpaka sasa bado haijakamilika licha ya kuwa kuna baadhi ya maeneo ya barabara hiyo imeanza kuharibika.

John kapinga mkazi wa eneo la Mateka naye alisema kuwa licha ya Kampuni hiyo kuanza kujenga barabara ya kutoka shule ya sekondari ya wasichana ya Songea hadi Matogoro haijakamilika nayo ujenzi wake kwa kiwango hicho cha lami.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Lukoro Construction Company Limited Mhandisi Harod Konga alipohojiwa alisema kuwa kampuni yake imekwisha anza kufanya matengenezo ya barabara hizo zenye urefu wa kilomita 8.6 ambazo zipo katika maeneo hayo tofauti.

Alisema kuwa ujenzi huo wa barabara kwa kiwango cha lami kwa sasa bado haujakamilika licha ya kazi ya ujenzi huo bado inaendelea hivyo amewataka wakazi wa Manispaa ya Songea kuondoa hofu na kuvuta subira wakati ujenzi huo ukiwa unaendelea na kukamilika kwa wakati uliopangwa.

Alizitaja barabara hizo zenye urefu wa kilomita 8.6 ni za kutoka Matogoro hadi FBC, shule ya wasichana ya Songea hadi Mateka, Mwembechai hadi Bombambili, eneo la Kituo kikuu cha Polisi hadi kituo cha daladala cha Mlyayoyo, Yapenda hadi eneo la Mitumbani na kwamba mradi huo wa ujenzi ulianza Julai mwaka jana na unatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu.


Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Manispaa ya Songea, Tina Sekambo alipohojiwa na mwandishi wetu ofisini kwake kuhusiana na ujenzi wa barabra hizo alisema kumekuwepo na malalamiko mengi kuhusiana na mkandarasi huyo kwamba anachelewesha kukamilisha ujenzi wa barabara hizo, lakini ofisi yake bado inafahamu kuwa mkataba unaonyesha kuwa Kampuni hiyo ya Lukoro inatakiwa kukabidhi barabra hizo ujenzi wake ukiwa umekamilika ifikapo Juni 30 mwaka huu.

No comments: