Wednesday, January 4, 2017

WANANCHI WALALAMIKIA UJENZI WA BARABARA

Na Kassian Nyandindi,         
Nyasa.

BAADHI ya Wananchi wanaoishi katika wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma wamelalamikia ujenzi wa barabara ya kutoka Mbinga mjini hadi Mbamba bay wilayani humo, iliyopo chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kutofuatilia kwa karibu ujenzi unaoendelea sasa, hali ambayo inasababisha barabara hiyo kufanyiwa matengenezo ya mara kwa mara.

Aidha walisema kuwa wanashangaa kuona ikifanyiwa matengenezo kwa mara ya pili na mkandarasi mwingine, wakati ni miezi michache tu imepita kulikuwa na mkandarasi ambaye alikuwa akiitengeneza.

Wameiomba serikali kupitia Wakala huyo wa TANROADS kuwabana wakandarasi wazembe wanaopewa kazi ya kujenga barabara wilayani hapa, ili kuepuka barabara hizo kufanyiwa matengenezo ya mara kwa mara jambo ambalo linaisababishia serikali hasara kubwa juu ya upotevu wa fedha za wananchi.


Pia walifafanua kuwa hata baadhi ya barabara zinazojengwa katika maeneo mbalimbali wilayani Nyasa ambazo zinasimamiwa na Wakala huyo, hazina ubora licha ya kutumia fedha nyingi ambazo zingeweza kuelekezwa katika miradi mingine ya maendeleo.

Hivi sasa wameutaka uongozi wa TANROADS mkoa wa Ruvuma kumfuatilia mkandarasi anayefanya ukarabati wa barabara inayoanzia Mbinga mjini kwenda kijiji cha Burma, kupitia kona hatari za Ambrosi  hadi daraja la mto Ruhekei kuhakikisha kwamba anasambaza kifusi anachomwaga barabarani kwa wakati na kiwango kinachotakiwa ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea kwa watumiaji wengine wa bara bara hiyo.

Simbert Ndunguru alieleza kuwa vifusi vinavyomwaga vinachelewa kusambazwa jambo ambalo linawafanya madereva wa magari hasa ya abiria kupita kwa taabu na wakati mwingine, hulazimika kupita upande ambao una bonde kubwa lenye kuhatarisha usalama wa magari hayo na abiria waliopanda kwa lengo la kukwepa vifusi vinavyomwagwa barabarani humo.

“Barabara hii ya Mbinga mjini hadi kwenda Nyasa ina kona nyingi ambazo ni hatari, huyu mkandarasi anapaswa kila anapomwaga kifusi akisambaze kwa wakati na sio kukiacha kwa muda mrefu bila kusambaza, kwani kumekuwa na usumbufu mkubwa wakati wa kupita na magari yetu”, alisema.

Naye Ally Komba aliongeza kuwa endapo mkandarsi huyo atachelewa kusambaza kifusi hicho katika barabara hiyo, ipo siku kuna hatari ya kutokea ajali hasa nyakati hizi za masika pale mvua zitakapoendelea kunyesha.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania mkoani Ruvuma, Razak Alinanuswe alipotafutwa ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya malalamiko hayo hakuweza kupatikana na simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

No comments: