Friday, January 20, 2017

MKUU WA WILAYA NAMTUMBO ATISHIWA KIFO

Na Kassian Nyandindi,      
Namtumbo.

MKUU wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Luckness Amlima ametishiwa kifo kwa maneno na mwananchi mmoja wa wilaya hiyo Gerold Haulle wakati alipokuwa akitekeleza zoezi la kuwahamisha wananchi wanaofanya shughuli za kibinadamu kwenye chanzo cha maji, ambacho ni tegemeo kubwa kwa hifadhi ya maji kwa wakazi wa mji wa Namtumbo.

Ofisa habari wa wilaya hiyo Yeremias Ngerangera alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 19 mwaka huu majira ya mchana wakati Mkuu huyo wa wilaya alipokuwa ofisini kwake na mwananchi huyo, akimhoji na kumtaka asitishe shughuli zake za kilimo ambazo amekuwa akizifanya kwenye chanzo kikuu cha maji ya mto Rwinga uliopo wilayani humo.

Ngerangera alifafanua kuwa hatua ya kumtaka Haulle aondoke kwenye chanzo hicho cha maji kimefuatia kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi na Mamlaka ya maji ya wilaya hiyo kwamba, amekuwa akikataa kuondoka kwenye chanzo na kukaidi maagizo yanayotolewa na serikali kuacha kufanya shughuli yoyote mita sitini kutoka kwenye maeneo yenye vyanzo vya maji.


Mkuu wa wilaya hiyo, Amlima amethibitisha kutokea kwa tukio hilo la kutishiwa kuuawa kwa maneno huku akiongeza kuwa taarifa zimefikishwa kituo kikuu cha Polisi wilayani Namtumbo kwa hatua zaidi.

“Tunamtaka mwananchi huyu aondoke kwenye chanzo hiki cha maji kwa sababu ni tegemeo kubwa kwa wananchi wengi wa mji wa Namtumbo, endapo akiendelea kufanya shughuli zake za kilimo ambazo zinaharibu mazingira ya chanzo hiki ni hatari kwa wananchi wangu kukosa huduma ya maji”, alisema Amlima.

Aliongeza kuwa licha ya kupewa kitisho hicho cha kifo ametoa wiki moja kwa kumtaka mwananchi huyo aondoke katika eneo hilo la chanzo na kuacha shughuli zake za kibinadamu, kwa kuwa suala hilo ni la kisheria na endapo ataendelea kukaidi atafikishwa mahakamani.


Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji alipoulizwa na mwandishi wetu alisema kuwa tukio hilo bado halijamfikia ofisini kwake na kwamba anafanya ufuatiliaji wa kina na kwamba atalitolea taarifa baadaye.

No comments: