Sunday, January 1, 2017

WAKULIMA NAMTUMBO WALALAMIKIA KUCHELEWA KWA PEMBEJEO ZA KILIMO

Na Yeremias Ngerangera,          
Namtumbo.

MGOMO wa wakulima wanaozalisha mazao ya aina mbalimbali katika kijiji  cha Namabengo  wilayani  Namtumbo  mkoa wa Ruvuma, umepatiwa ufumbuzi na Mkuu wa wilaya hiyo Luckness Amlima baada ya kwenda kijijini hapo kusikiliza madai yao na kuyapatia majawabu.

Madai hayo yaliyopatiwa ufumbuzi yalikuwa pamoja na wakulima hao kukataa kununua mbegu za ruzuku ya serikali kwa madai kuwa mbegu hizo, zimechelewa kuwafikia ambapo wananchi katika msimu wa mwaka huu tayari wamepanda katika mashamba yao kwa kutumia mbegu za asili walizokuwa nazo.

Vilevile baada ya kufikia muafaka juu ya jambo hilo, wakulima waliachiwa baadhi ya mbegu pamoja na mbolea za kukuzia huku wakiitaka serikali msimu ujao kupeleka pembejeo mapema ili isiweze kutokea tena hali kama hiyo.


Aidha Mkuu huyo wa wilaya, Amlima aliwataka wananchi kuzingatia utaratibu uliowekwa na serikali wa kuchukua mbolea za kupandia na kukuzia pamoja na mbegu ambazo tayari zimewekewa ruzuku.

Kadhalika madai ya wananchi hao kuchelewa kupata pembejeo hizo yanatokana baada ya serikali kubadilisha utaratibu ule wa awali, ambao ulizoeleka ambapo mawakala walikuwa wakiteuliwa kuzisambaza kwa wakulima na kusababisha kutowafikia walengwa.

Ambapo hivi sasa makampuni ndiyo yanayosambaza pembejeo hizo za kilimo kwa lengo la kupunguza malalamiko ya kutowafikia wananchi pembejeo, ili waweze kunufaika na ruzuku ya serikali na sio kwa wajanja wachache.


Naye kwa upande wake Ofisa kilimo wa wilaya hiyo, Stephen Mtunguja aliongeza kuwa msimu huu wa kilimo pamoja na mvua kuchelewa kunyesha lakini wakulima wanapaswa kuongeza jitihada ya kuzalisha mazao kwa wingi, ili kuweza kuondokana na matatizo ya njaa yanayoweza kujitokeza katika msimu ujao.

No comments: