Tuesday, January 3, 2017

ASKOFU MKUU WA JIMBO KUU LA SONGEA AWATAKA VIONGOZI KUTUMIA HEKIMA NA BUSARA KATIKA KULIONGOZA TAIFA

Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

ASKOFU Mkuu wa Kanisa katoliki Jimbo kuu la Songea mkoani Ruvuma, Damian Dallu amewataka viongozi hapa nchini kutumia hekima na busara katika kuliongoza taifa, kwa lengo la kuwatendea haki wananchi wanaowaongoza kwa ajili ya kudumisha amani na mshikamano.

Dallu aliyasema hayo juzi alipokuwa akihubiri katika ibada ya misa takatifu ya mkesha wa kuuaga mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2017 iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la kiaskofu la mtakatifu Mathias Kalemba mjini Songea.

Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Songea, Damian Dallu.
Alisema kuwa baadhi ya mataifa yameingia katika machafuko kutokana na viongozi wake kushindwa kutumia hekima na busara, katika kutatua changamoto na migogoro mbalimbali inayowakabili wananchi wake wanaowaongoza.

Kadhalika Askofu huyo amewataka viongozi hao kutumia mwaka mpya wa 2017 katika kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa hili, ikiwemo migogoro ya mapigano baina ya wakulima na wafugaji ambayo inasababisha umwagaji wa damu katika baadhi ya maeneo pale inapotokea.


Vilevile kiongozi huyo wa dini amekemea tabia inayofanywa na baadhi ya wananchi ya kukata viungo vya watu wenye matatizo ya ngozi (Albino) kwa imani kuwa vinaweza kuwasaidia kupata utajiri, pamoja na vyeo mbalimbali vya kisiasa jambo ambalo ameliita kuwa ni imani potofu na badala yake amewataka wawe na hofu ya Mungu.

Aidha amewataka waumini hao kuutumia mwaka huu katika kujiletea maendeleo ya kiuchumi, kumuomba Mungu ili aweze kuwajalia mafanikio mbalimbali ikiwemo hekima, afya njema, ulinzi na usalama, baraka za kimwili na kiroho kama ilivyokuwa kwa wana wa Israel.


Pamoja na mambo mengine alieleza kuwa waumini wengi hivi sasa wameyumbishwa kiimani, kutokana na kukabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo kutetereka kiafya na kwamba amewatahadharisha waumini hao kujiepusha pia na matapeli ambao wanapitia kwa mgongo wa dini.

No comments: