Thursday, January 5, 2017

SERIKALI KUJENGA KITUO CHA KUPOOZEA UMEME MAKAMBAKO HADI SONGEA

Na Kassian Nyandindi,       
Songea.

SERIKALI hapa nchini imesema kwamba inatarajia kujenga kituo cha kupoozea umeme gridi ya taifa kutoka Makambako mkoa wa Njombe hadi Songea mkoani Ruvuma, ambao utasafirishwa kwa lengo la kuondoa adha ya upatikanaji wa nishati hiyo muhimu katika mji wa Songea.

Kadhalika imeelezwa kuwa serikali imekuwa ikitambua kuwa upatikanaji wa umeme katika mkoa wa Ruvuma, umekuwa ni hafifu hivyo ili dhamira ya serikali ya uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo na vile vikubwa iweze kutimia ni lazima kuwepo na nishati ya umeme wa uhakika.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema hayo leo alipokuwa akizungumza na wananchi wa wilaya ya Songea vijijini huku akisisitiza kuwa umeme huo utasambazwa pia katika maeneo mbalimbali mkoani Ruvuma, kwa lengo la kuboresha na kuinua zaidi hali ya uchumi ya mkoa huo.


Majaliwa alisema kuwa serikali katika kutimiza hilo, inaendelea kusambaza umeme katika baadhi ya maeneo vijijini kupitia Wakala wake wa Umeme Vijijini (REA) kwa lengo la kuboresha viwanda hivyo vidogo vidogo.

Alisisitiza kuwa serikali haitalipa fidia kwa wananchi wa maeneo ambayo nguzo za umeme zitapita kwani malengo ya kufikisha nishati hiyo vijijini ni faida ya kuleta maendeleo kwa wote, hivyo wanapaswa kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa zoezi hilo ili liweze kuwa na ufanisi mkubwa.

Pia aliongeza kuwa Wakandarasi wanaondelea kujenga miundombinu ya umeme vijijini, waendelee kufanya kazi na kwamba serikali inakamilisha taratibu juu ya namna ya kuwalipa kwa kazi wanayofanya.

Katika tukio jingine, alipotembelea kituo cha afya Madaba kilichopo wilaya ya Songea vijijini mkoani hapa, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka wauguzi wa afya hapa nchini wasicheleweshe huduma kwa wagonjwa kwa lengo la kutaka wapewe hongo ndipo wamuhudumie mgonjwa.

Waziri huyo amesisitiza pia namna ya kutumia lugha nzuri kwa wagonjwa hao huku akieleza kuwa serikali itaendelea kuboresha huduma za afya na kukipandisha hadhi kituo cha afya Madaba kuwa hospitali kamili, ili kuweza kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Mapungufu ambayo hivi sasa yapo katika sekta ya afya, serikali imedhamiria kuyapatia ufumbuzi ili wananchi waondokane na adha wanayoipata sasa ya ukosefu wa dawa na vifaa tiba ili hatimaye waweze kuwa na afya bora ya kulitumikia taifa hili”, alisema.


Vilevile amezitaka halmashauri zote hapa nchini, kuendelea kuhamasisha Watanzania wajiunge na Mfuko wa Bima ya Afya (CHF) ili waweze kunufaika na matibabu kwa mwaka mzima na kwamba waondoe ukiritimba pale mwenye kadi hiyo ya bima anapokwenda kutibiwa. 

No comments: