Monday, January 30, 2017

SONGEA KUNA WATU 3,460 HAWAJUI KUSOMA KUANDIKA NA KUHESABU

Na Kassian Nyandindi,      
Songea.

IMEBAINIKA kuwa jumla ya watu wazima 3,460 wanaoishi katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma hawajui Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).

Kati ya watu hao wanaume ni 1,720 na wanawake ni 1,740 ambapo takwimu za idadi ya watu hao ni kuanzia wenye umri wa miaka 19 hadi 65.

Albano Midelo Afisa habari Manispaa ya Songea.
Albano Midelo ambaye ni Ofisa habari wa Manispaa hiyo, alisema kuwa elimu ya watu wazima katika Manispaa ya Songea inatekelezwa katika programu mbalimbali ambazo amezitaja kuwa ni Lanes, MUKEJA, KCM, KCK, Ndiyo Ninaweza na Ufundi na kwamba Manispaa ina idadi ya vikundi 64 vyenye washiriki 3,333 wakiwemo wanaume 1,493 na wanawake 1,840.

Midelo alisema kuwa licha ya changamoto zilizopo katika utekelezaji wa elimu ya watu wazima hapa nchini, ameyataja mafanikio ambayo yamepatikana katika elimu ya watu wazima katika Manispaa hiyo kuwa ni udahili wa wanafunzi wa kidato cha kwanza umepanda toka asilimia 84.6 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 98.5 mwaka 2016.


Alisema kuwa hali hiyo hutokana na utekelezaji wa elimu bila malipo, kupanda kwa ufaulu katika mitihani ya kidato cha nne na sita na uanzishwaji wa shule ya sekondari Emmanuel Nchimbi kwa ajili ya kidato cha tano na sita.

Mafanikio mengine ni ujenzi wa hosteli ya wasichana katika sekondari ya Matogoro na kumaliza tatizo la meza na viti vya kukali wanafunzi katika shule za sekondari zilizopo katika Manispaa ya Songea.

“Kwa mujibu wa matokeo ya sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2002, kulikuwa na watu wazima milioni 5.5 katika nchi nzima sawa na asilimia 32 ya watu ambao hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu”, alisema Midelo.


Alifafanua kuwa idadi ya watu wazima wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu imeendelea kuongezeka na kufikia zaidi ya watu milioni 10 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.

No comments: