Wednesday, January 25, 2017

CCM RUVUMA YAENDELEA KUVIBWAGA CHINI VYAMA VYA UPINZANI

Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma, kimeibuka na ushindi wa kishindo baada ya wagombea wake wa nafasi za udiwani kushinda katika kata mbili ya Tanga, iliyopo Manispaa ya Songea na Maguu wilayani Mbinga mkoani humo.

Uchaguzi huo ulifanyika Januari 22 mwaka huu ambapo katika kata ya Maguu msimamizi wa uchaguzi huo, Caspary Mahay alimtangaza Manfred Kahobela kuwa mshindi kupitia tiketi ya CCM baada ya kujizolea kura 2,355 na kumbwaga chini Bahati Mbele wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) aliyepata kura 1,717.

Katika kata ya Tanga msimanizi wa uchaguzi huo, Tina Sekambo alimtangaza Agaton Goliyama kwa tiketi ya Chama cha mapinduzi kuwa mshindi baada ya kupata kura 1,867 huku akiwashinda wagombea wa Chama cha demokrasia na maendeleo Vinitan Soko aliyepata kura 722, ACT Wazalendo Swaiba Mapunda kura 2 na Adolf Ngonyani wa CUF aliyepata kura 15.


Akizungumza mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi Manfredy Kahobela wa kaya ya Maguu wilayani Mbinga, aliwashukuru wananchi wa kata hiyo kwa kukiamini CCM na kwamba atahakikisha anashirikiana nao kwa karibu katika shughuli mbalimbali za maendeleo bila kujenga ubaguzi wa aina yoyote ile.


Naye Goliyama wa kata ya Tanga katika Manispaa ya Songea alieleza kuwa ushindi wa Chama cha mapinduzi alioupata, umedhihirisha wazi kuwa namna ambavyo Watanzania wanavyoendelea kukiamini chama hicho kutokana na utekelezaji wa yale ambayo yaliahidiwa yanavyofanyika kwa vitendo na serikali ya awamu ya tano.         

No comments: