Tuesday, January 17, 2017

MADUDU YA TASAF MBINGA YAITIA HASARA SERIKALI MAMILIONI YA FEDHA

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye.
Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

SERIKALI wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma imesema kuwa tokea ulipoanza mfumo wa kuziwezesha kaya maskini wilayani humo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu imepata hasara ya shilingi milioni 59,936,000 ambazo walikuwa wakilipwa walengwa hewa wasiokuwa na sifa.

Aidha kufuatia hali hiyo imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi milioni 26,474,000 katika kila awamu ya uhaulishaji fedha kwa kaya hizo maskini na wilaya imeweza kurejesha shilingi milioni 4,784,000 kutokana na walengwa hao kukosa sifa.

Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye alisema kuwa kufuatia kuwepo kwa tatizo hilo serikali imechukua hatua ya kumsimamisha kazi Mratibu wa TASAF wilaya, Ahsante Luambano ambaye anadaiwa kuzembea katika kusimamia majukumu yake ya kazi ipasavyo ili kupisha uchunguzi.


Nshenye alisema kuwa baadaye watakaofuatia katika zoezi hilo la kusimamishwa kazi ni watendaji wa kata na vijiji ambao nao katika maeneo yao yaliyokuwa yakitekelezwa miradi ya mfuko huo yataonekana kuwa na mapungufu hayo.

“Wilaya ya Mbinga inatekeleza mpango wa kunusuru kaya maskini ili kuboresha maisha yao na kujenga uelewa kwa wananchi wote juu ya kupiga vita umaskini, jumla ya vijiji 108 kati ya 170 vyenye wanufaika 10,307 waliwezeshwa katika mpango huu wa kunusuru kaya maskini”, alisema Nshenye.

Vilevile Nshenye alifafanua kuwa kiasi cha shilingi bilioni 3,574,427,206.54 kimetumika katika utekelezaji wa mpango huo hadi Disemba mwaka jana, kati ya shilingi bilioni 3,600,955,204.57 zilizopokelewa.


Aliongeza kuwa wilaya ilifanya zoezi la uhakiki na kubaini walengwa 191 wasiokuwa na sifa au kukosa vigezo vya kuendelea kuwemo kwenye mpango huo ambapo miongoni mwa sifa hizo ni pamoja na mlengwa kufariki, kuhama na kwamba katika kaya kuwa mjumbe wa serikali ya kijiji au mwenyekiti wa kitongoji katika eneo husika.

No comments: