Wednesday, January 4, 2017

WAZIRI MKUU AWATAKA VIONGOZI KUCHUKUA HATUA DHIDI YA WATOTO WASIOPELEKWA SHULE

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruvuma, Mhashamu Raphael Reuben Haulle akisalimiana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo katika uwanja wa ndege Songea mjini mkoani hapa, mara baada ya Waziri huyo kuwasili tayari kwa kuanza ziara ya siku tano ambapo atapata fursa ya kukagua na kuhimiza shughuli za maendeleo pamoja na kuongea na wananchi pamoja na watumishi wa serikali wa mkoa huo
Na Kassian Nyandindi,       
Songea.

VIONGOZI wa serikali mkoani Ruvuma, wameagizwa wahakikishe kwamba watoto wote walioandikishwa kuanza elimu ya awali, msingi na sekondari kwa mwaka huu wa masomo wanakuwepo shuleni mara shule zitakapofunguliwa Januari 9 mwaka huu.

Kadhalika wanapaswa kuchukua hatua dhidi ya watoto wenye umri wa kwenda shule ambao hivi sasa, wamekuwa wakishinda kwenye vituo vya mabasi (Magari ya abiria) ili waweze kwenda shule na kuweza kumaliza kabisa tatizo la utoro katika mkoa huo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ametoa agizo hilo leo akiwa mkoani Ruvuma katika ziara yake ya siku nne mara baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya mkoa iliyosomwa na Mkuu wa mkoa huo, Dkt. Binilith Mahenge Ikulu ndogo mjini Songea.

Amewaonya Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na miji hapa nchini kutekeleza kwa kusimamia kikamilifu mpango wa utoaji wa elimu bure kwa shule za serikali, ambao unatoa nafasi kwa vijana wengi zaidi kupata fursa ya kusoma kwani serikali imeshaondoa gharama zote ambazo zilikuwa kikwazo kwa baadhi ya familia.

Pamoja na agizo hilo Waziri Mkuu, Majaliwa ameagiza  pia jamii kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira kwenye maeneo yao ili waweze kuepuka hatari ya kutokea ukame hasa ukizingatia kuwa mkoa wa Ruvuma, unafaa kwa shughuli za kilimo na ni moja kati ya mikoa inayopata mvua za kutosha mwaka hadi mwaka.


Alisema kuwa suala la utunzaji mazingira sio la hiari bali ni la lazima kwa  kila mmoja wetu, kuhakikisha anawajibika katika kutunza mazingira yanayomzunguka kwenye eneo lake kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho na iwe ajenda ya  mara kwa mara   watendaji wa serikali pamoja na viongozi kuzungumzia jambo hilo pale wanapokutana na wananchi.

“Viongozi kila mnapokutana na wananchi jambo la kwanza ni lazima muwaeleze umuhimu wa kutunza mazingira yetu hali hii ninayoiona leo hapa Ruvuma, kwa kweli inaniogopesha sana kwani kawaida mwezi kama huu wakulima wengi wanakuwa wameshapanda lakini  mwaka huu ni tofauti kabisa”, alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Akizungumzia kuhusiana na shughuli za madini  Waziri Mkuu aliongeza kuwa serikali itaendelea kuwakaribisha wawekezaji katika suala zima la utafutaji na uchimbaji katika maeneo mbalimbali ya nchi, ili madini hayo yatakayopatikana yaweze kusaidia kuharakisha ukuaji wa uchumi na  kukua kwa pato taifa.

Vilevile aliziagiza mamlaka husika Ofisi ya madini Kanda ya Songea kupitia upya leseni zote za madini ili kuepusha migogoro kati ya wawekezaji wakubwa na wachimbaji wadogo kama ilivyowahi kutokea katika maeneo mengine jambo linapaswa kudhibitiwa mapema.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu huyo amewataka watendaji na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya kuendelea na ukusanyaji mapato katika halmashauri zao kwa kutumia mfumo wa mashine za EFD’S katika kukusanya mapato hayo ili kuepuka wizi na badala yake itasaidia kujenga udhibiti mapato yatakayopatikana.

Pia ameagiza kuwepo na matumizi sahihi ya fedha hizo zinazopatikana na kuhakikisha kwamba kila zinapokusanywa zinapelekwa benki kwa usalama zaidi badala ya kuwachia watu wanaokusanya ambao wanaweza kuzichezea au kuzielekeza katika matumizi mengine.

Sambamba na hilo, Waziri Mkuu amerudia agizo lake la kufuta posho kwa watumishi wa umma na madiwani badala yake ameelekeza fedha ambazo zilikuwa zikitumika kwa ajili ya kulipana posho, sasa   zielekezwe katika miradi ya maendeleo ya wananchi ili kusaidia kuboresha huduma mbalimbali za kijamii katika maeneo yao.

Alisema kuwa serikali  ya awamu ya tano inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara katika mkoa wa Ruvuma kwa kiwango cha lami, ili Watanzania waweze kusafiri kwa uhakika na kufanya shughuli zao za kiuchumi badala ya kutumia muda mrefu kusafiri katika barabara za vumbi.

“Baada ya kukamilika kwa barabara ya lami kutoka Songea hadi Tunduru kupitia wilaya ya Namtumbo kwenda Masasi mkoa wa Mtwara mpango wa baadaye wa serikali ni kujenga barabara ya lami kutoka Nachingwea, Rwangwa hadi Dar es Salaam kupitia Nangurukuru wilayani Kilwa barabara ambayo itapunguza umbali wa kutoka Songea kwenda Dar es Salaam na maeneo mengine.


Pia Waziri Mkuu amewahakikishia wananachi wa mkoa wa Ruvuma kwamba, serikali ipo katika hatua ya mwisho kukamilisha mchakato wa kuanzisha safari za ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Songea kwa kutumia ndege za shirika la ndege nchini ATCL.

No comments: