Friday, January 20, 2017

WAFANYABIASHARA SONGEA WAIOMBA SERIKALI KUWEKA UTARATIBU WA MAKAMPUNI YA TANCOAL ENERGY NA MANTRA KULIPIA KODI RUVUMA

Kamishna wa kodi za ndani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Elijah Mwandumbya akizungumza na wafanyabiashara wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kwenye ukumbi wa mikutano wa Songea Club uliopo mjini hapa, upande wa kushoto kwake ni Naibu Kamishna mkuu wa TRA Charles Kichele.
Na Mwandishi wetu,      
Songea.

WAFANYABIASHARA katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wameiomba serikali kuweka utaratibu kwa makampuni mawili yanayojishughulisha na uchimbaji madini mkoani hapa, kulipia kodi mkoani humo badala ya Dar es salaam ili yaweze kusaidia kupunguza makali ya shilingi bilioni 12 ambazo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Ruvuma imepangiwa kukusanya mwaka huu toka kwa wafanyabiashara hao.

Ombi hilo lilitolewa jana na wafanyabiashara hao kwenye mkutano uliofanyika baina yao na uongozi wa TRA makao makuu jiji Dar es Salaam, uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Songea Club uliopo mjini hapa.

Akichangia hoja kwenye mkutano huo mmoja wa wafanyabiashara hao Jaribu Mangoma alisema kuwa kutokana na kitendo cha serikali kuyaachia makampuni ya TANCOAL Eenergy inayojishughulisha na uchimbaji wa makaa ya mawe katika mgodi wa Ngaka uliopo kijiji cha Ntunduaro wilayani Mbinga na kampuni ya MANTRA inayofanya utafiti wa upatikanaji wa madini aina ya Urani, eneo la mto Mkuju wilayani Namtumbo ndiyo yanayochangia wafanyabiashara kukadiriwa kodi kubwa ambayo inawafanya baadhi yao wafilisike na wengine kufunga maduka yao.


Mfanyabiashara mwingine Omary Chika amelalamikia kuwepo kwa mrundikano wa kodi ambao umeonekana kuwa ni kero hivyo ameshauri Mamlaka ya mapato Tanzania, kuona umuhimu wa kuwa na tozo moja kwa kila mfanyabiashara ambayo itaunganisha kodi zote zinazotolewa hivi sasa kwa lengo la kupunguza kero na usumbufu wanaoupata wafanyabiashara hao.

Naye Emmanuel Kondowe pia ameishauri kufanyia marekebisho sheria ya kuwatoza wafanyabiashara wa nyumba za kulala wageni na hoteli kwa kulipa kodi kwa vigezo vya dola badala ya fedha ya kitanzania, jambo ambalo limekuwa likileta mgogoro baina ya wafanyabiashara hao na TRA ambayo imekuwa ikiwalazimisha walipe kwa mfumo wa dola wakati baadhi ya wateja wao hawana uelewa wa matumizi ya dola.

Kwa upande wake Katibu mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) mkoa wa Ruvuma Wilson Nziku alisema kuwa jamii ya wafanyabiashara hapa nchini, bado haina uelewa wa kutumia mashine za Kielektroniki (EFD) hivyo ameiomba serikali kutoa muda maalumu kwa TRA kutoa elimu ya kutosha huku akihoji pia kwa nini wafanyabiashara hao wameambiwa wanunue mashine hizo wakati serikali ilikwisha tangaza kwamba inatoa bure.

Kwa upande wake Naibu Kamishna mkuu wa Mamlaka ya mapato Tanzania, Charles Kichele amewataka wafanyabiashara hapa nchini kuona umuhimu wa kulipa kodi kwa wakati kwani kufanya hivyo ni kuijenga nchi yao kwa maendeleo sasa na vizazi vijavyo.

“Mkilipa kodi kwa wakati serikali itaweza kutengeneza miundo mbinu ya barabara, hospitali na taasisi mbalimbali za elimu ikiwemo vyuo vikuu nashauri pia wafanyabiashara tunzeni kumbukumbu zenu za biashara mnazofanya kwa kutumia mashine za EFD ambazo zitawasaidia kupunguza kero zinazojitokeza wakati wa kukadiriwa kodi”, alisema Kichele.

Kichele aliwapongeza wafanyabiashara wa mkoa wa Ruvuma kwa ushirikiano mkubwa wanaouonyesha baina yao na TRA kwa madai kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara wa maeneo mengine wamekuwa wakitoa michango ya kubomoa na sio kujenga huku akiongeza kuwa Mamlaka hiyo itahakikisha inatatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafanyabiashara hao mkoani hapa.

No comments: