Sunday, January 15, 2017

WAZIRI WA ARDHI ASISITIZA WANAOKAIDI MBINGA KULIPA KODI YA ARDHI WAFIKISHWE MAHAKAMANI

Dkt. Angelina Mabula, Naibu Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi.
Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

NAIBU Waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Dkt. Angelina Mabula ameuagiza uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, uhakikishe kwamba unatoa notisi kwa watu wote katika wilaya hiyo ambao hawajalipa kodi ya ardhi, ili waweze kulipa kwa wakati uliopangwa na kwa wale ambao watakaidi kulipa wapelekwe mahakamani.

Aidha alifafanua kuwa suala la kulipa kodi ya serikali ni lazima na sio hiari na kwamba katika wilaya hiyo kuna jumla ya shilingi milioni 500 zipo nje kwa wadaiwa wa kodi ya ardhi ambao wamemilikishwa viwanja kisheria na hawataki kulipa kodi husika kwa wakati.

Agizo hilo lilitolewa jana na Dkt. Mabula wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani hapa, akizungumza na wananchi wa Mbinga na viongozi wa wilaya kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa.

Dkt. Mabula alisisitiza pia katika kupunguza kero na migogoro ya ardhi ni vyema sasa viongozi husika ambao wamepewa dhamana ya kushughulikia masuala ya ardhi, wawafikie wananchi mara kwa mara kwenye maeneo yao na kutatua matatizo hayo yaliyopo kwa wakati.


“Pangeni ratiba mbalimbali ya kuwafikia wananchi pale walipo, tukifanya hivyo tutaweza kupunguza kero na migogoro hii ambayo inaleta usumbufu katika jamii na kurudisha nyuma maendeleo ya taifa hili”, alisema.

Vilevile aliutaka uongozi wa wilaya ya Mbinga kuwalipa fidia wananchi wote ambao hawajalipwa fidia zao mara baada ya kutwaliwa viwanja vyao na kwamba kwa wale pia ambao wanadai hati miliki za viwanja vyao wapewe kwa wakati ili kuondoa migogoro na malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

“Hakikisheni hati zote za kawaida na kimila zinatolewa kwa wakati na pia wananchi wale ambao hawajapata hati zao nawashauri kama wana ofa zipelekeni halmashauri ili muweze kupata hati zenu na pale panapotakiwa kulipa gharama husika lipeni ili muweze kupata hati zenu”, alisisitiza Dkt. Mabula.

Pia aliwataka viongozi wa wilaya wahakikishe wanatenga maeneo ya kuchungia mifugo ili kuepukana na migogoro ya ardhi, watu kupigana na kupoteza maisha jambo ambalo hatimaye linapoteza nguvu kazi ya taifa hili.

Kadhalika aliongeza kwa kuwataka wananchi waache vitendo vya kuharibu mazingira ya vyanzo vya maji na kuchoma moto misitu kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha kukosa mvua na kukaribisha hali ya ukame.

Hata hivyo katika ziara hiyo ya Naibu Waziri Dkt. Mabula aliweza kusikiliza kero na migogoro mbalimbali kwa wananchi wa wilaya ya Mbinga na kuweza kuipatia ufumbuzi kwa kuwataka viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia masuala ya ardhi kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria za nchi na sio vinginevyo.

No comments: