Friday, August 21, 2015

ALIYEONGOZA KUNDI LA KUVAMIA WAANDISHI WA HABARI APANDISHWA KIZIMBANI

Na Mwandishi wetu,
Mbinga.

DANIEL Komba (53) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ruanda kata ya Ruanda mkoani Ruvuma, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya wilaya ya Mbinga mkoani humo kwa kosa la kumshambulia Mwenyekiti wa kijiji hicho na waandishi wa habari waliokwenda kijijini hapo, kutekeleza majukumu yao ya kikazi.

Mwendesha mashtaka wa Polisi Inspekta, Seif Kilugwe alisema hayo mbele ya Hakimu wa Mahakama ya wilaya hiyo, Issa Magori kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Agosti 3 mwaka huu majira ya saa 7 mchana.

Inspekta Seif alisema kwamba, Komba akiwa na wenzake alimshambulia Mwenyekiti wa kijiji, Deograsias Haulle na kumjeruhi eneo la usoni kitendo ambacho kilimsababishia maumivu makali mwilini mwake.


Alifafanua kuwa siku ya tukio kulikuwa na waandishi wa habari wa mkoa wa Ruvuma, Kassian Nyandindi anayeandikia magazeti ya kampuni ya Businesstimes, Aden Mbelle na Pastory Mfaume wa radio Jogoo FM nao walinusurika kujeruhiwa katika vurugu ambazo zilizojitokeza kijijini hapo.

Mwendesha mashtaka huyo aliendelea kuieleza Mahakama kuwa, hali hiyo ilijitokeza wakati wanahabari hao walipokwenda kutekeleza majukumu yao ya kikazi, kuandika habari za tukio la kufungwa kufuli Ofisi za kata ya Ruanda na baadhi ya wananchi, ambao majina yao bado hayajapatikana hivyo wakati wakikamilisha kazi yao ya kuandika habari, ndipo walishambuliwa na kundi la watu ambalo lilikuwa likiongozwa na mshtakiwa Komba.

Kadhalika aliongeza kuwa upelelezi shauri hilo bado haujakamilika na kwamba watuhumiwa wengine ambao walihusika katika tukio hilo, bado hawajapatikana wanaendelea kutafutwa na pale watakapopatikana watafikishwa mahakamani ili waweze kujibu tuhuma inayowakabili mbele yao.


Hata hivyo mshtakiwa Komba alikana mashtaka, yupo nje kwa dhamana ambapo shtaka hilo litatajwa tena mahakamani hapo Septemba 3 mwaka huu.

No comments: