Tuesday, August 25, 2015

DOKTA MAGUFULI KUTIKISA RUVUMA AGOSTI 30 MWAKA HUU

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

DOKTA John Pombe Magufuli, ambaye ni mgombea Urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hapa nchini anatarajiwa kupokelewa na maelfu ya wananchi na wapenzi chama hicho, katika kijiji cha Igawisenga wilayani Songea mkoani humo akitokea mkoa wa Njombe tayari kwa kuanza kampeni ya chama hicho ndani ya mkoa huo.

Waandishi wa habari waliozungumza na Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya kampeni ya CCM hapa Ruvuma, Ramadhan Kayombo alisema kuwa Dokta Magufuli na msafara wake unatarajiwa kupokelewa Agosti 30 mwaka huu, majira ya asubuhi katika kijiji hicho.

Kayombo alisema Chama hicho, kimejipanga kikamilifu katika kuhakikisha kwamba mgombea huyo, wabunge na madiwani ndani ya mkoa huo wanafanyiwa kampeni zenye ustaarabu na sio vinginevyo.


Dokta Magufuli anatarajia kufanya ziara yake ya kampeni mkoani Ruvuma katika wilaya ya Nyasa, Mbinga, Songea, Namtumbo na Tunduru ambako atamaliza ziara yake Septemba 2 mwaka huu na kuendelea mkoani Mtwara.

Mwenyekiti huyo wa maandalizi ya kampeni ya CCM mkoani humo, alifafanua kuwa wananchi wengi wanaimani na chama hicho na kwamba wanahitaji kumuona mgombea huyo na kumsikiliza sera zake.


Alisema kwa kuwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kwenye mikutano ya hadhara, itakayofanyika wakati Dokta Magufuli atakapokuwa amewasili hapa mkoani Ruvuma huku akiwaomba kuwa na mshikamano wa pamoja katika kuhakikisha CCM kwenye uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu kinapata ushindi wa kishindo kwa mgombea nafasi ya urais, wabunge na madiwani.

No comments: