Saturday, August 8, 2015

KATIBU WA CHAMA CHA MAPINDUZI NYASA ALALAMIKIWA NA WANACHAMA WAKE

Abdulrahman Kinana.
Na Muhidin Amri,
Nyasa.

WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiendelea kukamilisha mchakato wa kura za maoni hapa nchini, hali imekuwa si shwari kwa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, ambapo baadhi ya wanachama wake wameonekana kukatishwa tamaa kwa kile kinchodaiwa kuwa Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Grayson Mwengu amekuwa akitengeneza makundi ndani ya chama hicho wilayani humo, jambo ambalo linahatarisha ustawi wake.

Kufuatia hali hiyo wanachama wa chama hicho walisema kuwa, huenda CCM ndani ya wilaya hiyo katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, kisifanye vizuri katika nafasi ya Diwani, Mbunge na Rais kutokana na mambo yanayofanywa na katibu huyo ambayo yanaashiria kukipeleka chama kubaya.

Walifafanua kuwa tayari baadhi ya wanachama wameanza kujiondoa ndani ya chama na kujiunga na vyama vya upinzani, kwa kile kinachoelezwa kuwa wamechoshwa  na vitendo vya dharau na kukosekana kwa umoja na mshikamano uliokuwepo kwa muda mrefu na haya yote kukosekana huko, kumesababishwa na katibu huyo.


Kadhalika kwa nyakati tofauti Alex Shauri, Christopher Challe na Steven Maluka walisema Mwengu, ni mtu mwenye kiburi na asiyependa ushirikiano na wenzake ndani ya chama badala yake amekuwa na tabia ya kuwakumbatia baadhi ya wagombea wenye fedha na kutotenda haki kwa wengine, ambao wanaonekana hawana fedha jambo ambalo linalalamikiwa na wanachama wengi wa chama hicho wilayani Nyasa.

Alex Shauri alieleza kuwa kutokana na hali hiyo kunauwezekano mkubwa kwa CCM jimbo la Nyasa kutofanya vizuri kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni, kwa kila alichoeleza kuwa baadhi ya wanachama tayari wameonesha kukatishwa tamaa juu ya mwenendo na utendaji kazi wa katibu huyo wilayani humo.

“Binafsi nasema kuna kila sababu kwa uongozi wa makao makuu ya chama chetu kulifanyia kazi suala hili, hasa kuchukua hatua mapema kumuondoa huyu mtu kabla hajakiharibu chama kwa kiasi kikubwa, wanachama tumekatishwa tamaa na uongozi huu wa wilaya ndani ya CCM kila tunapofika ofisini kwake ni mtu mwenye dharau, kiburi na amekuwa mtu ambaye hatoi ushirikiano wa kutosha”, alisema Shauri.

Shauri ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri kuu taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi wilayani humo, ameendelea kuuomba uongozi husika ngazi ya mkoa na taifa kwa ujumla kulifanyia kazi suala hilo, ili kuweza kukinusuru chama ikiwemo kumuhamisha kituo hicho cha kazi katibu huyo ambaye muda mwingi amekuwa akijigamba kwamba ameletwa Nyasa, kwa kazi maalumu na katibu mkuu wa CCM Abdulrhaman Kinana.

“Yawezekana kweli ameletwa na bosi wetu Kinana, pamoja na hilo sasa anachotakiwa ni lazima ajenge heshima na mahusiano mazuri na wanachama wenzake, ukizingatia kwamba shughuli za chama zinahitaji mshikamano wa pamoja”, alisema Shauri.

Naye Christopher Challe alisema kuwa tangu Mwengu alipoletwa kufanya kazi wilayani Nyasa, amekuwa ni sehemu ya matatizo kwa kutengeneza makundi na kuwagawa wanachama kitendo ambacho kinahatarisha ustawi wa chama na kukiweka katika wakati mgumu.

Kwa upande wake waandishi wa habari walipomfuata Mwengu ofisini kwake, ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya madai hayo alikataa kuzungumzia hilo, huku akiongeza kuwa yeye hana muda wa kuzungumza na vyombo vya habari.


“Mimi kwa sasa sina muda wa kuzungumza na waandishi wa habari, kwanza siwafahamu na mmetoka wapi au kawatuma nani”, alisema Katibu huyo wa CCM wilaya ya Nyasa, akainuka katika kiti chake na kutoka nje ya ofisi yake huku akiwaacha waandishi wa habari wakiwa wameshikwa na butwaa.

No comments: