Tuesday, August 25, 2015

NAMTUMBO WAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE KATIKA UTEKELEZAJI MIRADI YA MAJI

Na Muhidin Amri,
Namtumbo.

HALMASHAURI ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa miradi mikubwa minne ya maji iliyogharimu shilingi bilioni 2.7 ikiwa ni sehemu ya mikakati katika utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo, kwa kipindi cha mwaka 2010 hadi sasa 2015. 

Miradi hiyo ya maji imejengwa kwenye kijiji cha Milonji, Mkongo njalamatata, Mkongo gulioni na Magazini sambamba na uchimbaji wa visima vifupi 12 vya maji ambavyo tayari wananchi wa maeneo hayo wameanza kuvitumia, jambo ambalo linawafanya waweze kuondokana na adha ya kutafuta maji umbali mrefu kama ilivyokuwa hapo awali.

Afisa mipango wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Tekra Nyoni alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake mjini Namtumbo huku akiongeza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo, kumetokana na ushirikiano wa kutosha kati ya serikali na wananchi wa maeneo hayo.


Nyoni alisema, mbali na hayo halmashauri hiyo pia imejenga zahanati katika kijiji cha Mawa, Nambecha, Namtumbo mjini, Mageuzi, Mchomoro na Namanguli kwa gharama ya shilingi milioni 250 fedha ambazo zimetokana na vyanzo mbalimbali vya mapato yake ya ndani.

Vilevile halmashauri ya Namtumbo, inaendelea na ujenzi wa jengo la upasuaji kwa akina mama wajawazito katika hospitali ya wilaya hiyo na jengo jingine katika kituo cha afya Lusewa ambalo mara baada ya ujenzi wake kukamilika, litasaidia akina mama hao kupatiwa huduma ya matibabu kwa urahisi hasa kwa kata jirani.

Ujenzi huo umefuatia kutokana na hospitali ya wilaya hiyo, kukosa jengo la huduma za upasuaji kwa akina mama hao ambapo wengi wao hulazimika kufuata huduma hiyo umbali wa kilometa 100 hospitali ya mkoa Songea, iliyopo mjini hapa.

Pia serikali imeona umuhimu wa ujenzi huo kufanyika haraka, kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi wake hasa baada ya kubaini ongezeko kubwa la idadi ya wanawake, wanaohitaji kupata huduma hiyo.

Afisa mipango huyo aliongeza kuwa halmashauri hiyo, katika bajeti yake ya mwaka 2014 na 2015 pia imeshaanza kutenga kiasi cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara kiwango cha lami, ambapo barabara moja yenye urefu wa kilometa 2 tayari imejengwa kwa shilingi milioni 600 mjini Namtumbo.

Kwa upande wa idara ya elimu ya msingi na sekondari, Nyoni alifafanua kwamba katika kuhakikisha walimu wake wanaishi katika mazingira mazuri wametumia shilingi milioni 160, kwa ajili ya ukarabati wa nyumba nane za walimu wa shule za msingi na kwa upande wa sekondari zimejengwa nyumba katika vijiji vya Lisimonji, Lukimwa, Corido, Utwango, Nasuli na Mageuzi kwa gharama ya shilingi milioni 210.


Mbali na hayo Halmashauri ya Namtumbo, katika kuinua shughuli zake za kilimo hasa kwa mazao ya biashara tayari imegawa miche ya mikorosho 29,000 kwa wakulima wake, katika kata ya Magazini, Lusewa na Mchomoro na kwamba wanatarajia kusambaza miche mingine katika msimu ujao wa kilimo cha zao hilo hasa kwenye maeneo ambayo korosho inastawi vizuri.

No comments: