Saturday, August 15, 2015

GAUDENCE KAYOMBO ANYANG'ANYA VIFAA VYA MATANGAZO ALIVYOKINUNULIA CHAMA CHA MAPINDUZI MBINGA BAADA YA KUSHINDWA KWENYE UCHAGUZI KURA ZA MAONI

Gaudence Kayombo.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MBUNGE wa Jimbo la Mbinga Gaudence Kayombo, ambaye aliingia katika mchakato wa uchaguzi wa kura za maoni jimbo la Mbinga vijijini mkoani Ruvuma, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) amewashangaza wanachama wa chama hicho baada ya mbunge huyo kwenda ofisi za CCM wilayani humo kunyang’anya vifaa vya matangazo, ambavyo ni vipaza sauti baada ya kushindwa kwenye kinyanga’nyiro hicho cha kura za maoni uliofanyika Agosti Mosi mwaka huu.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti mjini hapa, wanachama hao walisema kuwa Kayombo alifanya hivyo baada ya kuwasili katika ofisi hizo za chama Agosti 14 mwaka huu majira ya asubuhi, akionekana mtu mwenye hasira.

“Huyu Mbunge alipowasili pale ofisi za chama alitushangaza sana, alikuwa mtu mwenye hasira huku akizungumza kwa ukali anataka vifaa vyake vya matangazo ambavyo alikinunulia chama, huku akitamka maneno kwamba ameamua kufanya hivyo kwa sababu viongozi wa chama wilaya hawamtaki”, walisema.


Aidha walifafanua kuwa kitendo alichofanya Kayombo ni cha aibu, kwani yeye akiwa mwanachama wa CCM anapaswa kuendelea kukisaidia chama kwa mambo mbalimbali na sio kufanya kitendo kama hicho, cha kunyang’anya vitu ambavyo alikipatia chama.

Walibainisha kuwa Mbunge huyo baada ya kuona ameangukia pua kwenye kinyang’anyiro cha kura za maoni zilizofanyika hivi karibuni, muda mwingi alikuwa akiwalaumu viongozi wa chama hicho wilaya ya Mbinga akisema kuwa ndiyo waliochangia aweze kudondoka katika mchakato huo.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Mbinga, Zainabu Chinowa alithibitisha hilo na kueleza kuwa wao kama chama wamesikitishwa na kitendo hicho ambacho hawakutegemea Kayombo kama angeweza kufanya hivyo.

“Huyu mtu ametushangaza sana, hili jambo alilofanya ni aibu yake yeye mwenyewe tunajua kitendo hiki cha kutunyang’anya vipaza sauti ni hasira zake alizonazo baada ya kushindwa, kwenye uchaguzi wa kura za maoni”, alisema Chinowa.


Hata hivyo CCM kwa upande wa jimbo la Mbinga vijijini kulikuwa na wagombea ubunge nane ambao waliingia kwenye mchakato huo wa kura za maoni uliofanyika Agosti Mosi mwaka huu ambao ni; Martin Msuha aliyeongoza kwa kupata kura (13,354), Gaudence Kayombo (12,068), Humprey Kisika (545), Dokta Silverius Komba (3,941) na Deodatus Ndunguru (7,060) matokeo hayo yalitangazwa Agosti 3 mwaka huu majira ya saa 5:45 usiku na Katibu wa Chama hicho wilaya ya Mbinga, Zainabu Chinowa.

No comments: