Friday, August 7, 2015

MWANDISHI WA HABARI KAPINGA AIBUKA KIDEDEA KATIKA KURA ZA MAONI

Cresensia Kapinga.
Na Muhidin Amri,
Songea.      

MWANDISHI wa habari mwandamizi, Cresensia Kapinga (40) ameibuka kidedea baada ya Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Ndilimalitembo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,  kumchagua kwa kura nyingi kupitia kura za maoni zilizofanyika hivi karibuni, kuwa mgombea kwa nafasi ya udiwani kupitia tiketi ya chama hicho Oktoba 25 mwaka huu.

Kapinga amefanikiwa kupata kura 527, dhidi ya wagombea wenzake Hashimu Fungafunga aliyepata kura 127, Francis Lungu kura 111 na Issa Kiwaneke aliyepata kura 27 ambapo huyu ni mwandishi wa pili mkoani hapa kushinda kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM.

Mbali na Kapinga mwandishi wa habari mwingine ni, Dustan Ndunguru ambaye naye ameshinda kupitia mchakato huo wa kura za maoni kwa nafasi ya udiwani katika kata ya Kihungu, wilayani Mbinga mkoani humo.


Akizungumza mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi, Kapinga alieleza kuwa iwapo atachaguliwa kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu, atahakikisha anapambana na watu wote hususani watumishi wa umma ambao wanakwamisha kwa makusudi maendeleo ya wananchi wake, katika kata ya Ndilimalitembo.

Kapinga alifafanua kuwa amelazimika kutoa kauli hiyo, kufuatia baadhi ya wanachama wa chama hicho ambao walifurika katika ofisi za CCM kata ya Ndilimalitembo, kumpongeza kwa ushindi alioupata huku wengine wakisema sasa wanamatumaini mapya kwa mgombea huyo na kuanza kumpatia majukumu ya kufuatilia mapato na matumizi ya miradi mbalimbali iliyotekelezwa ndani ya kata hiyo, ambayo wananchi hawajasomewa na kupewa taarifa kamili juu ya utekelezaji wake.

Alisema suala la kuwasomea wananchi mapato na matumizi ya fedha za miradi yao ni jambo la lazima na sio vinginevyo, hivyo watendaji wa mitaa na kata kwa ujumla atahakikisha wanatekeleza hilo kwa wakati, ili kuondoa malalamiko yasiyokuwa na msingi.


Pia aliwaomba wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kujenga ushirikiano wa pamoja na kuhakikisha wanamchagua Diwani, Mbunge na Rais wa CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao huku wakiacha ushabiki ambao unaweza kukiweka chama pabaya.

No comments: