Tuesday, August 25, 2015

NALICHO: TUMIENI KALAMU ZENU KUTANGAZA FURSA ZA MAENDELEO

Na Muhidin Amri,
Ruvuma.

WAANDISHI wa habari mkoani Ruvuma, wamepewa changamoto ya kutumia kalamu zao ipasavyo kwa ajili ya kuandika na kutangaza fursa mbalimbali za maendeleo ndani ya mkoa huo, hatua ambayo itaweza kuwavutia wawekezaji wengi wa ndani na nje ya nchi kwenda kuwekeza mkoani humo.

Mbali na hilo wametakiwa kutumia nafasi waliyonayo kuhamasisha wananchi kupenda kushiriki katika shughuli za kimaendeleo, hususani kwa zile za kujitolea ili kuweza kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.

Chande Nalicho ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, alitoa rai hiyo alipokuwa akikagua ujenzi wa chumba cha upasuaji akina mama wajawazito kinachojengwa na serikali katika hospitali ya wilaya hiyo, huku akiongeza kuwa ujenzi huo utatoa fursa kwa akina mama hao kuweza kupata huduma za matibabu kwa ufanisi zaidi.


Nalicho alisema kuwa kazi ya kutangaza fursa zilizopo au kuhamasisha wananchi kupenda kujiletea maendeleo siyo ya serikali pekee, bali kila mmoja wakiwemo waandishi wa habari wanakila sababu ya kutumia kalamu zao ipasavyo katika kuhamasisha jamii, ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kadhalika amewataka wanahabari mkoani humo kuandika habari za uchunguzi kwani ndizo zinazoibua kero nyingi zinazoikabili jamii, badala ya kutumia muda mwingi kuandika habari za wanasiasa ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo wanaochangia kuleta umaskini na migogoro ya hapa na pale hususani kwa wananchi waishio vijijini.


Hata hivyo amewasihi watumishi wa serikali na makundi mengine katika jamii, kutobaki nyuma katika kupigania maendeleo bali kila mmoja ahakikishe anakuwa chachu ya upatikanaji na mafanikio katika nyanja hiyo muhimu, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

No comments: