Monday, August 31, 2015

DOKTA MAGUFULI: SERIKALI ITAJENGA BARABARA YA MBINGA MBAMBA BAY BAADA YA UCHAGUZI MKUU


Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

MGOMBEA urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dokta John Magufuli amesema kuwa, mara baada ya kufanyika uchaguzi mkuu Oktoba 25 mwaka huu serikali itaanza mchakato wake wa kujenga barabara ya kutoka wilaya ya Mbinga kwenda Mbamba bay wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, kwa kiwango cha lami.

Sambamba na hilo alieleza pia serikali itaunganisha umeme wa gridi ya Taifa kutoka Makambako mkoa wa Njombe hadi hapa Ruvuma.

Dokta Magufuli alisema hayo leo alipokuwa akihutubia mamia ya wananchi wa wilaya hiyo, ambao walikusanyika kumsikiliza  kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya CCM mjini hapa.

“Ndugu zangu nataka niwahakikishie haya ninayosema nilazima niyatekeleze, Tanzania ijayo ya Magufuli haitafanya mzaha juu ya kuleta maendeleo ya wananchi, nchi hii najua ina fedha nyingi sana lazima zitumike ipasavyo kwa manufaa ya jamii”, alisema Dokta Magufuli.


Alisema kuwa katika kufanikisha hilo, atahakikisha viongozi ambao wanatabia ya kufuja fedha za wananchi anawachukulia hatua za kisheria ikiwemo pia na kuziba mianya hiyo ya ufujaji, ili maendeleo yaweze kupatikana.

Kadhalika alifafanua kuwa endapo Watanzania watamchagua kwenda Ikulu kuiongoza nchi hii, atawatumikia ipasavyo ili waweze kuwa na maisha bora kwani waliowengi wamekuwa wakinyanyasika kutokana na kukosa haki zao za msingi.

“Nataka niwatumikie Watanzania waliowengi ambao wananyanyasika, ndio maana leo hii nipo hapa nawaomba kura zenu kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya kweli, ninawaomba wanambinga tufanye mabadiliko yaliyobora kwa kukichagua Chama Cha Mapinduzi ili Magufuli aweze kuwaletea maendeleo”, alisema.

Pamoja na mambo mengine, mgombea huyo aliongeza kuwa anafahamu wananchi wamekuwa na kero mbalimbali ambazo zinasababishwa na watumishi waliopo madarakani katika Halmashauri za wilaya, mkoa hadi taifa hivyo atakapoingia madarakani atawashughulikia ili kuweza kuondoa kero hizo.

Hata hivyo alibanisha kuwa katika kutekeleza hilo, ataanzisha Mahakama ya kuwashughulikia mafisadi wote wanaotafuna fedha za wananchi ili kuweza kukomesha hali hiyo, isiweze kuendelea.

No comments: