Wednesday, August 12, 2015

GAUDENCE KAYOMBO AFUKUZWA NA WAPIGA KURA WAKE GARI LANUSURIKA KUPIGWA MAWE

Katibu wa Halmashauri kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Nape Nnauye. 
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

GAUDENCE Kayombo ambaye ni mgombea nafasi ya ubunge kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Mbinga vijijini mkoani Ruvuma, amejikuta akiendelea kuwa katika wakati mgumu kwa madai kwamba baadhi ya wananchi wa kijiji cha Paradiso kata ya Ruanda kumfukuza kijijini hapo huku wakimwambia kwamba, wananchi hawataki kusikia taarifa ya kurudia tena kufanya uchaguzi wa kura za maoni katika kata hiyo.

Tukio hilo la aina yake limetokea usiku wa leo, Agosti 12 mwaka huu majira ya saa 2:20 wakati mgombea huyo akionekana katika maeneo ya kijiji hicho akiwa na gari lake ikidaiwa anapita kwenye kata hiyo kuhamasisha wapiga kura, wajitokeze kupiga kura ya maoni kwenye matawi yao kesho, Agosti 13 mwaka huu.

Hasira za wananchi hao zinafuatia baada ya CCM mkoani hapa, kutoa taarifa kwamba kutafanyika marudio ya uchaguzi wa kura za maoni katika kata ya Ruanda na Kihangimahuka kwenye jimbo hilo, baada ya matokeo ya awali kufutwa kwa sababu mbalimbali zilizojitokeza katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni kwenye jimbo hilo.

Marudio ya uchaguzi huo yanatokana pia na Kayombo kulalamikia juu ya hali hiyo kutoridhishwa nayo, huku wagombea wenzake wakibaki kumshangaa wengine wakisema amekosa kazi ya kufanya na huenda ni tamaa ya madaraka aliyonayo au hajakomaa kisiasa.


Nimezungumza na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi kata ya Ruanda, John Ndimbo amethibitisha kutimuliwa kwa Kayombo katika kijiji hicho usiku wa leo na kuongeza kuwa, yeye hana taarifa kamili juu ya marudio ya uchaguzi huo.

“Hivi sasa ninavyokuambia dakika 20 zilizopita, Kayombo amefukuzwa na wananchi wa kijiji cha Paradiso baada ya kukutwa akihamasisha kwa mmoja wa katibu tawi, kwamba kesho kutafanyika marudio ya uchaguzi wa kura za maoni katika kata hii,

“Wananchi walishikwa na hasira baada ya kumuona na kumwambia hawataweza kupiga kura tena na hawamtaki, wengine walianza kushika mawe na fimbo za miti wakitaka kupiga gari lake na hatimaye aliondoka na kutokomea kusikojulikana’, alisema Ndimbo.

Ndimbo alisema wanamshangaa Kayombo akipita kuhamasisha watu wapige kura wakati kazi hiyo ni ya viongozi wa chama na sio mgombea, hivyo wanamashaka naye huenda anatamaa ya madaraka.

Kadhalika uchunguzi uliofanywa na mtandao huu, kwa upande wa kata ya Kihangimahuka ambako uchaguzi unatarajiwa kurudiwa hali imekuwa tete ambapo katibu kata wa CCM wa kata hiyo, Hallad Ndimbo amezungumza na mwandishi wetu akisema kuwa wananchi hawapo tayari juu ya suala hilo.

“Binafsi sina taarifa kamili juu ya marudio ya uchaguzi huu wa kura za maoni katika kata yangu, nasikia tu taarifa za mtaani ambazo sio rasmi labda kama ningepewa hata barua na uongozi wa chama wilaya, ningeweza kuzungumzia ukweli juu ya jambo hili”, alisema Ndimbo.

Kwa upande wake alipotafutwa mgombea, Kayombo ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya mkasa huo aliokumbana nao katika kijiji cha Paradiso na viongozi hao wa CCM katika kata hizo, hakuweza kupatikana na simu yake lilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

Pamoja na mambo mengine Katibu wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Ruvuma, Verena Shumbusho alipoulizwa kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi juu ya kurudiwa kwa uchaguzi huo wa kura za maoni kwenye kata hizo kupitia tiketi ya chama hicho, alithibitisha hilo akisema ni kweli kutafanyika marudio ya uchaguzi huo kesho Agosti 13 mwaka huu.


Hata hivyo CCM kwa upande wa jimbo la Mbinga vijijini kulikuwa na wagombea ubunge nane ambao waliingia kwenye mchakato huo wa kura za maoni uliofanyika hivi karibuni ambao ni; Martin Msuha aliyeongoza kwa kupata kura (13,354), Gaudence Kayombo (12,068), Humprey Kisika (545), Dokta Silverius Komba (1,289), Edesius kinunda (2,355), Deodatus Mapunda (2,532), Benaya Kapinga (3,941) na Deodatus Ndunguru (7,060) matokeo hayo ambayo yalitangazwa Agosti 3 mwaka huu majira ya saa 5:45 usiku na katibu wa chama hicho wilaya ya Mbinga Zainabu Chinowa.  

No comments: