Saturday, August 29, 2015

TAMCU TUNDURU YAPITISHA MAKISIO YAKE BILA MABADILIKO

Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKUTANO mkuu wa Chama kikuu cha ushirika wilaya ya Tunduru mkoa wa Ruvuma (TAMCU – LTD) kimepitisha bila ya kuyafanyia mabadiliko, makisio ya mapato na matumizi shilingi milioni 345 katika msimu wa ununuzi wa mazao mwaka 2015 na 2016, huku kukiwa na ongezeko la asilimia 0.01 ikilinganishwa na makisio ya mwaka uliopita.

Aidha katika mkutano huo, wajumbe waliridhia kuuzwa kwa hisa 500,000 kati ya hisa zake 720,000 ili fedha zitakazopatikana zitumike kulipia deni la chama hicho, ambalo wanadaiwa na benki ya CRDB.

Maamuzi hayo yalifikiwa na Wajumbe wa mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa ofisi za chama hicho, zilizopo katika mtaa wa Kalanje mjini hapa ambapo maamuzi hayo yalifikiwa pia kutokana na chama hicho, kukua kwa mapato yake.


Sambamba na hayo wajumbe hao walipitisha maamuzi yao yenye makisio ya kununua tani 9,400 za korosho, zenye thamani ya shilingi bilioni 9 ikiwa ni tofauti na msimu uliopita vyama vya ushirika wilayani humo, vilikusanya tani 8,000 zenye thamani ya shilingi bilioni 9.6.

Awali akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya mkutano huo Meneja mkuu wa TAMCU wilayani Tunduru, Imani Kalembo alisema chama chake kimefikia uamuzi wa kuongeza makisio hayo kwa lengo la kuwawezesha wakulima, waweze kufanya palizi na kupulizia dawa katika mikorosho yao kwa wakati.


Naye Mwenyekiti wa chama hicho, Issa Kambutu alipokuwa akifungua mkutano huo aliwaomba wajumbe na wanachama wa chama hicho kutoa ushirikiano wakati wa utekelezaji wa majukumu husikandani ya chama, huku Afisa ushirika wa wilaya hiyo Yusuph Kwilimbea akipongeza jitihada zinazofanywa na chama kwa kuzingatia taratibu, sheria na kanuni za ushirika ili kuepukana na malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

No comments: