Saturday, August 29, 2015

NAMATUHI SONGEA KUNUFAIKA NA KILIMO CHA UMWAGILIAJI

Na Muhidin Amri,
Songea.

WAKAZI wa kijiji cha Namatuhi Halmashauri ya Songea vijijini mkoani Ruvuma, watanufaika na kilimo cha umwagiliaji zao la mpunga baada ya halmashauri ya wilaya hiyo, kukamilisha ujenzi wa skimu ya kilimo hicho.

Halmashauri ilichukua maamuzi ya kujenga miundombinu hiyo, baada ya kuona wakazi hao wanashindwa kunufaika ipasavyo na shughuli za kilimo cha zao hilo kutokana na kukosekana kwa miundombinu husika ya uzalishaji mpunga, licha ya juhudi kubwa walizokuwa wakizifanya za uzalishaji wa zao hilo kila mwaka.

Sixbert Kaijage, ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Songea vijijini alisema hayo wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi kijijini humo, akizungumza na wakulima wa zao hilo.


Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa, awali wananchi wa kijiji cha Namatuhi walikuwa wakitumia njia za kizamani kuzalisha zao hilo kwa kutegemea mvua za msimu, ambapo baada ya wananchi kuibua wazo la kutaka mradi huo wajengewe miundombinu ya kisasa ya umwagiliaji, ndipo halmashauri hiyo ikatekeleza hilo na sasa wanatumia njia bora za kilimo kuzalisha mapunga.

Kaijage alisema wilaya yake bado ina ardhi kubwa na yenye rutuba inayofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula na biashara, na kwamba haitumiki vizuri kutokana na wakulima wengi kuendelea na kilimo cha zamani cha kuhama hama huku akiwataka waanze kubadilika na kuachana na kilimo cha mtindo huo ambacho hakina tija kwa karne hii ya sayansi na tekinolojia.


Aliongeza kuwa kuanzia msimu wa mwaka huu 2015 na 2016 atahakikisha wakulima wa wilaya ya Songea vijijini, wanatumia mbinu za kilimo bora ili waweze kuzalisha kwa wingi mazao yao.

No comments: