Friday, August 7, 2015

MOHAMED LAWA ALALAMIKIWA TUNDURU KWA KUMBEBA MGOMBEA

Na Steven Augustino,
Tunduru.

SEKRETARIETI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma, imeridhia kumtoa katika mchakato wa kusimamia uchaguzi wa kura za maoni, katibu wa chama hicho wilayani Tunduru mkoani humo, Mohamed Lawa ikiwa ni lengo la kukiondoa chama katika mgogoro uliojitokeza kati ya katibu huyo na wagombea ubunge jimbo la Tunduru Kaskazini.

Akitangaza maamuzi hayo hivi karibuni, Katibu wa Chama hicho mkoani hapa, Verena Shumbusho alisema kuwa maamuzi hayo yamefikiwa baada ya kujiridhisha uwepo wa hoja za msingi, zilizotolewa na wagombea hao.

Shumbusho alifafanua kuwa maamuzi hayo yametokana na sekretarieti ya mkoa huo kuketi na kujadili hilo na kuchukua maamuzi ya kumteua Katibu wa jumuiya ya wazazi mkoani Ruvuma, Haji Tajiri ambaye alikuwa miongoni mwao kubakia Tunduru ili aweze kuendelea kusimamia mchakato huo hali ambayo iliweza kuleta matumaini kwa wagombea na kukubali, kuendelea na mikutano ya kujinadi katika jimbo hilo.


Akijibu maombi ya wagombea hao ya kukitaka chama kuchukua hatua dhidi ya viongozi wote, watakaobainika kushiriki kugawa kadi za chama pasipo kuwa na sifa pia waondolewe kwenye kinyang’anyiro cha kuwa mgombea kwa nafasi ya udiwani au ubunge.

Zainabu Kalikalanje, Mussa Manjaule pamoja na makatibu wa matawi wa CCM kutoka Nakapanya, Mchororo na Majengo wilayani Tunduru nao walitaka wachukuliwe hatua za kinidhamu kutokana na kukiuka taratibu, sheria na miongozo ya chama.

Shumbusho baada ya kupokea hilo, alisema atatuma kamati ya maadili kwenda huko kwa ajili ya kulifanyia kazi.

Alisema kuwa katika mchakato huo, wagombea nane kati ya tisa waligomea kuendelea na mchakato huo wakidai kubaini uwepo wa upendeleo wa ugawaji kadi zisizokuwa halali kwa wanachama wa chama hicho wilayani humo, ikiwa ni lengo la kutaka kumbeba mgombea waliyemtaja kwa jina la Injinia Ramo Makani.

Katibu huyo alisema katika taarifa ya wagombea hao, ambayo ilitumwa kwenda ofisi ya Chama Cha Mapinduzi mkoa na Taifa, ilibainisha kuwa katika mgao wa kadi hizo kulikuwa na kata ambazo zilipewa kadi chini ya 200 huku matawi mengine yakipewa zaidi ya kadi 700 idadi ambayo ilikuwa hailingani na uhalisia husika.

Alisema katika taarifa hiyo, makada hao walitolea mfano wa mgao wa kadi 1000 ambazo inadaiwa kupelekwa kwenye tawi la Cheleweni, ambako anatokea Injinia Ramo.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wetu, wagombea hao Hassan Kungu, Issa Mtuwa, Omary Kalolo, Athuman Nkinde, Shaban Uronu, Moses Kaluwayo, Michael Matomora na Rashid Mohamed walisema kuwa wapo tayari kumuunga mkono mgombea yeyote miongoni mwao isipokuwa Injinia Ramo Makani.

No comments: